Wananchi wilayani Makete mkoani Njombe wametahadharishwa kukaa umbali wa kuanzia mita 200 kutoka kilipo kituo cha kupigia kura ili kuacha shughuli mbalimbali katika kituo husika ziendelee kwa mujibu wa sheria za uchaguzi
Kauli hiyo imetolewa na Msimamizi msaidizi wa uchaguzi jimbo la Makete Bw Rafael Kalongola kwenye mahojiano maalum na eddy blog kuhusu jinsi ofisi yake ilivyojipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika bila matatizo yoyote na kulinda amani na utulivu uliopo
Kalongola Amesema ni kosa kisheria kukizingira kituo cha kupigia kura mara baada ya mwananchi kupiga kura, hivyo ili kuepusha matatizo yasiyo ya lazima ikiwemo kuchukua hatua za kisheria ni lazima wananchi waondoke kwenye vituo hivyo, na wataruhusiwa kurejea baadae kujionea matokeo mara baada ya kubandikwa
Katika hatua nyingine amewataka wananchi kuondokana na dhana potofu kuwa kukaa kwao kwenye vituo kutasaidia kuzuia uibaji wa kura ambao amesema haupo, kwa kuwa tume imejipanga vizuri kukabiliana na hilo kupitia sheria zake za uchaguzi
"Matokeo yakiwa tayari mawakala wa vyama watakuwa na nakala za matokeo, msimamizi wa kituo baada ya watu kupiga kura kutakuwa na zoezi la uhesabuji kura wa wazi, nakala zitakuwepo, matokeo yatabandikwa, sasa ndugu mwandishi hata ukifikiria mwenyewe huo wizi utatoka wapi?" amesema
Zoezi la kupiga kura linatarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, ambapo wananchi wa jimbo la Makete wameomba kujitokeza kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka na kujiepusha na vitendo vyovyote vitakavyoibua vurugu wakati wa uchaguzi
