Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Freeman Mbowe akihutubia wananchi wa Makete
Wananchi wapenda mabadiliko wilayani Makete mkoani Njombe wametakiwa kulinda kura zao baada ya kupiga na kukaa umbali wa mita 200 toka kilipo kituo walichopigia kura
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA Freeman Mbowe wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya mabehewani Makete mjini jana ambapo pia aliambatana na mgombea urais wa chama hicho Edward Lowassa
Mbowe amesema haiwezekani kwa hali ilivyo sasa nchini wananchi wakapiga kura na kwenda nyumbani kwa kuwa kumekuwa na viashiria vya kukosekana uaminifu ambavyo vitasababisha wizi wa kura
"Wangapi mtakubali kupiga kura na kwenda nyumbani? Mnataka nani awalindie kura zenu? Mnataka muwaachie CCM wawalindie?, Sheria inasema hivi ukishapiga kura nenda umbali wa mita 200 toka kilipo kituo, subiri matokeo yako hapo, huo ndio utaratibu, iweje leo waseme tuende nyumbani baada ya kupiga kura?" amesema Mbowe
Hivi karibuni tume ya taifa ya Uchaguzi NEC imewataka wananchi kupiga kura na kuondoka vituoni kuelekea majumbani kama njia mojawapo ya kuepusha vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kujitokeza, jambo ambalo limekuwa likipingwa na vyama mbalimbali vya siasa hasa vya upinzani