Makete yazungumzia kuhusu kulinda kura

Kauli ya kuondoka kwenda nyumbani au kwenye shughuli za kila siku mara baada ya mwananchi kupiga kura, ama kubaki umbali wa mita 200 toka kilipo kituo cha kupigia kura, imeendelea kuleta utata kwa wananchi wa wilaya ya Makete mkoani Njombe

Kufuatia suala hilo mwandishi wetu amezungumza na Afisa Uchaguzi jimbo la Makete Mwl Gregory Emmanuel (pichani) kupitia kipindi cha Morning Alarm kinachorushwa na kituo cha Green Fm 91.5, na kusisitiza kuwa endapo mtu akimaliza kupiga kura aondoke kituoni na akaendelee na majukumu yake

Afisa huyo amesema hakuna haja ya kukaa umbali wa mita 200 kwa kuwa suala hilo litasababisha mkusanyiko ambao umekatazwa kisheria hivyo wanaweza kwenda kuendelea na majukumu yao na ikifika muda wa kutangaza matokeo wakafika kituoni na kujionea matokeo ya wagombea wao

"Kuna vituo vingine vipo ndani ya makazi ya watu, hata wakiondoka umbali wa mita 200 bado wapo ndani ya makazi yao, hiyo ni changamoto na tunaikubali" amesema Gregory

Amesema wananchi wasiweke mikusanyiko isiyo ya msingi wakati wa kumaliza kupiga kura, na badala yake watu wawaamini mawakala wanaowakilisha vyama vyao, kwa kuwa wamewaamini na kuwapa ridhaa, na endapo watu watakiuka taratibu zilizowekwa watachukuliwa hatua za kisheria

Kumekuwa na hali ya sintofahamu inayosababishwa na baadhi ya wagombea kuwataka wananchi kulinda kura baada ya kupiga kwa kukaa umbali wa mita 200 toka kilipo kituo, huku tume ya taifa ya Uchaguzi NEC ikisisitiza wananchi kuondoka na kwenda nyumbani baada ya kupiga kura, na sheria ya uchaguzi ikitamka kuwa wananchi waondoke umbali wa mita 200 toka kilipo kituo wasubirie matokeo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo