Magufuli atoa kauli juu ya askari aliyekufa kwenye msafara wake


Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kwa Jeshi la Polisi,  kufuatia kifo cha askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, aliyepata ajali wakati akiongoza msafara wake. 
 
Taarifa iliyotolewa jana na CCM kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa, Dk.  Magufuli alipokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha askari huyo, F.4946 PC. Essaya ambaye alipata ajali juzi wakati akiongoza msafara wa mgombea huyo wa urais na kupoteza maisha eneo la Ubungo Mataa, jijini Dar es Salaam.
 
Dk. Magufuli katika salamu zake za rambirambi alizomtumia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, alisema:  “Kwa hakika, nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za kifo cha F. 4946 PC. Essaya ambacho kimetokea baada ya kupata ajali ya kugongana na pikipiki (Bodaboda) iliyoingilia msafara wangu uliokuwa ukitokea Lugalo kwenda Vingunguti, jijini Dar Es Salaam."
 
Aidha,  alimuomba Inspekta Mangu, kumfikishia salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na rafiki wa marehemu. 

"Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu ya uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi. 

Pia namuombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, kazi ya Mungu haina makosa,”  ilisema taarifa hiyo ikimnukuu, Dk. Magufuli.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo