Mwenyekiti wa ZEC
Mwanasheria nguli nchini Profesa Chris Peter Maina, amesema kuahirishwa kwa uchaguzi huo ni hasara kubwa kwa nchi kwani fedha zilizotumika kuandaa uchaguzi huo ni za walipakodi ambao watalazimika kubeba gharama nyingine zaidi.
Alisema kilichofanywa na Zec kimeteteresha imani ya wananchi kwa tume hiyo kwani Mwenyekiti wake alipaswa kuwachukulia hatua mara moja makamishna waliokiuka sheria na kanuni siku ya kupiga kura.
“Zec ilitakiwa iwe na uwezo wa kukamata watu waliovunja sheria na kuwachukulia hatua, siyo kusubiri siku zimepita ndipo wanayasema haya na kufuta matokeo…naona kama hawakuzingatia sheria kwa kutotoa taarifa mapema,” alisema.
Aliongeza: “Zec wamepoteza imani ya wananchi na fedha za walipakodi ambazo zingelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.”
Hata hivyo, alisema kwa sasa itamlazimu Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Wawakilishi ili kuidhinisha muda wa kuendelea kukaa madarakani hadi hapo uchaguzi mwingine utakapofanyika.