Kingunge aongeza tena madongo mengine mapya kwa CCM

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Kombare ­Mwiru amesema historia itamhukumu kwa uamuzi alioufanya wa kuihama CCM, baada ya kuituhumu kuvunja katiba wakati wa uteuzi wa mgombea wa urais wa chama hicho. 

Kingunge ambaye mapema wiki iliyopita alitangaza kujitoa CCM, alisema ametoa mchango mkubwa kwa nchi na chama na kwamba uamuzi alioufanya ni sahihi kwa sasa baada ya kutoridhishwa na uvunjaji taratibu. 

Akizungumza na Tido Mhando katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na televisheni ya Azam TV, Kingunge alisema hawezi kubabaika na maneno mabaya yanayosemwa juu yake baada ya kuondoka CCM. 

Mwanasiasa huyo ambaye ni moja ya waumini wakuu wa ujamaa, alisema baada ya kutangaza uamuzi wa kujiondoa kuna baadhi ya watu walimtupia lawama kuwa amefanya makosa kwa sababu yeye ni alama ya chama. 

Kingunge alisema huu ni wakati wake muafaka kuikosoa CCM, lakini viongozi wa CCM wapo kimya na kukimbilia kutoa madai kuwa utaratibu ulifuatwa. 

Aliendelea kuutupia lawama uongozi wa juu wa CCM akiwemo mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kwa kushindwa kukemea kauli zisizofaa kama za “goli la mkono” zinazoashiria kuwa chama hicho kinataka kushinda hata kwa kuvunja katiba ya nchi. 

Alipoulizwa iwapo kujitoa kwake kumetokana na Lowassa kujiondoa CCM, Kingunge alisema kilichomuondoa ni kuvunjwa katiba ya chama na uamuzi wa kujitoa angeufanya hata kama Lowassa angeteuliwa kugombea urais ndani ya chama hicho. 

Tangu CCM imalize mchakato wa kumteua mgombea wa urais Julai 12 mwaka huu, kwa kumteua Dk John Magufuli, Kingunge alikuwa ni kinara wa makada wa chama hicho waliojitokeza mara nyingi hadharani kuituhumu kuwa ilivunja taratibu na katiba. 

Hata hivyo, mkongwe huyo hakuwa miongoni mwa vigogo wa kwanza kujiondoa CCM, hata baada ya kada aliyekuwa akimuunga mkono Lowassa kung’atuka CCM, Julai 28 na kujiunga Chadema na kupatiwa nafasi ya kugombea urais. 

Alipoulizwa Lowassa ataletaje mabadiliko wakati ametoka ndani ya CCM miezi miwili iliyopita, Kingunge alisema alimuunga mkono mgombea huyo akiwa ndani ya CCM kwa sababu anajua historia yake ya “uchapakazi na mwendo wake wa kasi” ambao unaweza kutatua matatizo ya wananchi. 

Alisema pamoja na kuwa miongoni mwa watu wanaotaka mbadiliko, anachukizwa na baadhi ya watu kulihusisha jambo hilo na Lowassa wakati ni la wananchi. 


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo