Kijana mmoja aliyetambulika kwa jina la Juma Rajabu, 23, mkazi wa Kijiwe Samli Wilaya ya IIala, Dar nusura auawe baada ya kula kichapo maeneo ya Buguruni Sheli, hali iliyofanya afikishwe na polisi Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam kwa matibabu.
Chanzo chetu kilisema kijana huyo alipigwa hadi kupoteza fahamu na wabaya wake waliodai kuwa aliwaibia na baada ya kichapo waliamini kuwa amefariki dunia.
“Vijana wale baada ya kumpiga naye kupoteza fahamu wakajua kuwa wamemuua, hivyo wakamuacha palepale hadi polisi wa doria walipofika na kumchukua,” kilisema chanzo ambacho hata hivyo haikuelezwa alituhumiwa kuiba nini.
Habari zinasema baadhi ya watu wanaomfahamu kijana huyo walifikisha habari nyumbani kwao wakidai kuwa ameuawa na maiti yake ipo Hospitali ya Amana, hivyo maandalizi ya mazishi yakafanyika.
“Jumamosi asubuhi familia yao baada ya kupata taarifa za ‘msiba’ waligawana majukumu, wapo waliokwenda kuchumba kaburi, wapo waliokwenda kununua sanda na upishi wa chakula ulifanyika,”alisema mama mzazi wa kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Tatu Mohamed (65).
Bi Tatu alisema kila aliyepewa jukumu lake lilifanya na waliokwenda Hospitali ya Amana walipofika walimkuta Juma akiwa hai ila akiwa ameumizwa na kushonwa nyuzi kadhaa sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Watu waliokwenda Amana walituarifu kwa simu kwamba Juma hajafariki dunia, hivyo shughuli za msiba zikasitishwa mara moja na watu wakatangaziwa na wakatawanyika.
Alipohojiwa na gazeti hili Juma alisema kuwa alipigwa na na watu asiowajua baada ya kusingiziwa kuwa ni mwizi.