Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imesema karatasi za kupigia kura kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu,zinatarajiwa kuwasili nchini Septemba 29, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuleta vifaa vya uchaguzi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa ununuzi na ugavi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Eliu Njaila amesema matayarisho ya vifaa vya kupigia kura yanaenda vizuri, ambapo amebainisha kwamba baadhi ya vifaa muhimu vinavyohitajika vimeshaanza kuwasili.
Amevitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni vituturu (vibanda) vya kupigia kura, mihuri na vitabu ambavyo vimeshaanza kusambazwa mikoani ambapo ya shilingi Bilioni 41.6 kwa ajili ya vifaa hivyo tayari yamekamilika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo,karatasi za kupigia kura pekee ndizo zinazoagizwa kutoka nje ambapo amesema vifaa vingine muhimu vimepatikana hapa nchini baada ya kutangazwa zabuni.
Aidha, bwana Njaila amewataka wananchi kutokuwa na hofu kuhusu upatikanaji wa vifaa hivyo ambapo amesema vyote vitapatikana na hakutakuwa na upungufu.