RAIS Jakaya Kikwete, amesema hamshangai mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.John Magufuli kwa kukosoa utendaji kazi wa Serikali yake katika mikutano yake ya kampeni inayoendelea.
Rais Kikwete, alitoa kauli hiyo juzi, wakati akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi ya NDI yenye uhusiano na Chama cha Democratic, IRI yenye uhusiano na Chama cha Republican, IFES na United States Institute of Peace (USIP) mjini Washington nchini Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu mjini Dar es Salaam jana, ilisema Rais Kikwete anaunga mkono mwenendo wa kauli za Dk. Magufuli kwa sababu kila kiongozi anapoingia madarakani anakuwa na aina yake ya uongozi.
“Wamepata kuja watu kwangu,wakaniambia mgombea wetu wa CCM anashutumu na kusahihisha Serikali yangu na utendaji wake kwenye mikutano ya kampeni. Niliwaambia hivi anavyofanya mgombea wetu ni jambo sahihi kabisa,lazima afanye hivyo.
“Niliwaambia nchi yetu, inahitaji mawazo mapya na mwelekeo mpya ulio tofauti na uongozi wangu. Niliwaambia tusiporuhusu jambo hilo kufanyika, nchi yetu itabakia pale pale ambako nimeifikisha mimi.
“Haya yatakuwa na makosa makubwa kwa sababu nchi yetu lazima isonge mbele kwa mawazo mapya,uongozi na staili mpya ya uongozi.
“Haya ndiyo anayosema mgombea wetu. Vinginevyo ni jambo lisilokuwa na maana kubadilisha uongozi kama hatuko tayari kukubali, kila kiongozi lazima awe na staili yake ya uongozi na namna ya kuongoza na kuendesha nchi yetu,” alisema.
Katika mikutano yake Dk. Magufuli amekuwa akieleza namna asivyoridhishwa na uwepo wa huduma mbovu katika sekta mbalimbali ikiwamo afya na maji, hali inayowafanya wananchi waendelee kutaabika.
Dk. Magufuli amekuwa akishangaa kuona dawa zinakosekana katika hospitali za Serikali huku dawa hizo zikipatikana katika maduka binafsi na kuahidi kupambana na majizi na mafisadi.
Mgombea huyo pia amekuwa akishangaa pale ambapo baadhi ya watumishi wanapoharibu aidha kwa kuiba fedha za umma au uzembe kazini kuhamishwa vituo vya kazi, badala ya kufukuzwa na kushitakiwa.
Atamani kupumzika
Katika hatua nyingine,Rais Kikwete alisema anatamani muda uende kwa kasi zaidi ili akabidhi madaraka kwa rais wa awamu ya tano.
“Natamani muda uende nikabidhi madaraka kwa rais wa tano ili nipate muda wa kumpumzika,baada ya kazi ngumu ya miaka 10 ambayo ni kama mzigo mkubwa,”alisema Rais Kikwete.