Mwimba kwaya afia kwenye mkutano wa kampeni za CCM huko Lindi

Mkazi wa mtaa wa Mbuyuni kata ya Ng’apa Jimbo la Lindi Mjini, Fatu Jega anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 28, amefariki dunia ghafla akiwa kwenye mkutano wa kampeni.
 
Fatu alifariki dunia Septemba 21, mwaka huu saa 10:00 jioni wakati wa kampeni ya mgombea udiwani kata ya Ng’apa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwanaidi Mbungo.
 
Alifariki dunia muda mfupi baada ya kumaliza kuimba nyimbo za uhamasishaji watu kwenye mkutano huo uliofanyika eneo la Lukwania katika kata hiyo.
 
Baada ya muda wa kuimba nyimbo za uhamasishaji kumalizika, mwanakwaya huyo aliketi chini pamoja na wenzake na kuanza kusikiliza sera kutoka kwa viongozi mbalimbali wa chama hicho.
 
Wakati baadhi ya viongozi wakiendelea na hotuba za utangulizi, ndipo mwanakwaya huyo aliposikika akisema anawaona watu wa ajabu wakipita mbele ya uso wake na punde si punde, akaanguka chini na kupoteza fahamu.
 
Mkutano huo wa uzinduzi wa kampeni, pia ulihudhuriwa na  mgombea ubunge wa Jimbo la Lindi Mjini, Selemani Kaunje.
 
Kitendo hicho kiliufanya mkutano huo kusimama na baadhi ya watu waliokuwapo wakambeba Fatu na kumkimbiza Zahanati ya Ng’apa kwa matibabu.
 
Hata hivyo, ilibainika kuwa mwanakwaya huyo alikuwa tayari ameaga dunia.
 
Mganga Mkuu wa Zahanati ya Ng’apa aliyejitambulisha kwa jina moja la Dk. Ally, alithibitisha kutokea kwa kifo cha mwanakwaya huo.
 
“Ndugu mliomsindikiza, huyu mtu ameshafariki muda mrefu. Urudisheni nyumbani mwili wake kwa taratibu nyingine za mazishi,” alisikika Dk. Ally akiwaambia wana-CCM waliokuwa wamempeleka katika zahanati hiyo, hali iliyoamsha vilio na simanzi miongoni mwao.
 
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Lindi Mjini, Mukhusini  Ismail, alisema Chama kimempoteza mtu aliyekuwa tegemeo ndani ya chama chao hususan katika kipindi hiki cha kampeni.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo