Msafara
wa mgombea urais kupitia
chama cha ACT Wazalendo
umezuiwa kwa muda na
wananchi wa Wilaya ya
Nachingwea, wakidai kuwa na
wao wanahitaji baraka kutoka
kwa mgombea huyo baada ya
kuzikosa kwa muda mrefu.
Kitendo cha kusimamishwa
katika eneo la soko la Nachingwea Mjini, kilimlazimu mgombea
Anna Mghwira, kuwahutubia akiwa barabarani huku akilakiwa na
umati mkubwa wa watu.
Kama vile haitoshi wananchi hao walimlazimisha mgombea huyo
kwenda kwenye kiwanja cha Nachingwea, ili kuwaeleza ni kwavipi chama chake kitapambana kuondoa umasikini unaowakabili.
“Nashuka tuandamane hadi huko kiwanjani wapiga kura wangu”
alisema mgombea huyo na kuandamana na wananchi hao
kuelekea kwenye viwanja vilivyoko karibu na soko la Nachingwea.
Ilimchukua muda wa saa moja mgombea huyo kueleza sera za
chama chake kwa wananchi wa Nachingwea na kuahidi kuzifanyia
kazi kero mbalimbali mara watakapompa ridhaa ya kuongoza
Tanzania.
Mghwira alianza kwa kuelezea vipaumbele vya ACT Wazalendo
endapo kitaingia madarakani.
Alivitaja vipaumbele hivyo ni
pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii, ambapo aliwaahidi
wananchi hao kuingizwa katika mfumo utakaowawezesha
kujiwekea akiba na hivyo kuwasaidia katika matibabu na hata
maisha ya baadaye.
“Katika utawala wangu kila mmoja atafaidika na mifuko hiyo ya
hifadhi ya jamii. Sitakuwa tayari kusikia Mtanzania anashindwa
kujihudumia wakati wa ugonjwa au wakati akiwa amezeeka na
hafanyi kazi tena,” alisema.
