Magufuli adhihirisha kuwa haumwi kwa kupiga pushup jukwaani

Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, jana aliwaacha hoi wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika mkutano wake baada ya kufanya mazoezi jukwaani kwa kupiga pushapu saba ili kudhihirishia kile alichodai kuwa mbali na kutoa ahadi nzuri na kuinadi ilani ya chama chake, pia yungali na nguvu ya kutosha kuwatumikia Watanzania baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
 
Dk. Magufuli alipiga pushapu hizo jana na kuuacha hoi umati uliofika kushuhudia kampeni zake wakati akihutubia kwenye viwanja vya Changarawe vilivyopo Karagwe Mjini mkoani Kagera. 
 
Hapo alikuwa njiani pia kuelekea Wilaya ya Ngara kwa ajili ya kampeni nyingine alizofanya jana jioni katika jimbo la nane mkoani humo.
 
Dk. Magufuli alisema ana nguvu za kutosha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tofauti na wagombea wengine ambao alisema hawawezi hata kuruka ruka jukwaani wakati wakihutubia.
 
“Mimi nina nguvu na kama mnataka niwathibitishie naweza kuruka ruka hapa jukwaani na hata mkitaka nipige pushapu naweza kupiga... au mnataka niwaonyeshe kwamba mimi nina nguvu nipige pushapu?” alihoji na kuitikiwa na wananchi 'ndiyooo'.
 
Baada ya wananchi hao kumtaka afanye hivyo, Dk. Magufuli aliinama kwenye jukwaa alilokuwa akihutubia na kupiga pushapu saba za haraka, hali iliyoibua shangwe kubwa kutoka kwa maelfu ya wananchi waliofika kumsikiliza huku wengine wakiangua kicheko.
 
Miongoni mwa wagombea wanaoonekana kuchuana kwa karibu zaidi na Magufuli kutokana na wingi wa watu wanaojitokeza karibu katika kila mkutano wa kampeni ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye pia anawakilisha muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF). Wengine wa nafasi ya urais wanaotarajiwa kuchuana na Magufuli ni Hashim Rungwe wa Chaumma, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Fahmy Dovutwa wa UPDP,  Chifu Lutasola Yemba, wa ADC, Maximillian Lymo, wa TLP, Fahmy Dovutwa, wa UPDP na Janken Ksambala, wa NRA.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo