Afya ya Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Mashariki ambaye pia ni mwanasheria Mabere Marando,
imeanza kuimarika na leo alifanyiwa vipimo kadhaa katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa.
Marando alifikishwa hospitalini hapo Jumapili jioni akiwa
hajitambui baada ya kuugua ghafla akiwa nyumbani kwake na
kulazwa katika jengo la tiba la magonjwa ya upasuaji wa moyo,
katika wodi maalum za kulipia FF4 chumba namba 2.
Akizungumza leo Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili John Stephen,
alisema hali ya Marando inazidi kuimarika huku akiendelea kupatiwa matibabu na madaktari
bingwa.
“Leo amefanyiwa vipimo kadhaa na hali yake sasa inaridhisha, familia bado haipo radhi
kuzungumza chochote na isingependa kuonana na vyombo vya habari kwa sasa na iwapo atapata
nafuu ataweza kuzungumzia nini zaidi kinamsumbua,” alisema Stephen.
Mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema Marando
alifikishwa hospitalini hapo akiwa na hali isiyoridhisha.
“Hana tatizo la moyo bali anaonekana kuzidiwa baada ya kufanya kazi kupita kiasi.
Si mgonjwa
sana ila anasumbuliwa kiasi anaonekana amefanya kazi kwa muda mrefu na hivyo kukosa wasaa
wa kupumzika, madaktari wamempatia matibabu maalum kwa ajili ya kuirudisha afya yake katika
hali ya kawaida.