Dkt Willbroad Slaa atangaza rasmi kuachana na siasa za vyama

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa ameeleza Watanzania kwamba amestaafu siasa baada ya chama hicho kumpokea aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Aidha amesema kwamba pamoja na yeye kushiriki katika mazungumzo ya kumuingiza Lowassa baada ya kushawishiwa na Askofu Gwajima alisema kwamba misingi aliyoiweka ya kumpokea Lowassa haikuzingatiwa hasa kutokana na ukweli kuwa Lowassa hajajisafisha  na  pia hawezi kukwepa kashfa ya Richmond.
Dk Slaa aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wa takribani saa mbili katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam kuwa Lowassa si kiongozi anayefaa kuwa rais wa nchi.
Alisema kwamba kiongozi huyo anmayewania uongozi wa taifa hili ana makandokando mengi ya vitendo vya rushwa na kwamba ni mhusika namba moja katika kashfa ya Richmond iliyomwondoa madarakani Februari 2008.
Tangu Julai 28, wakati Lowassa alipoanza kuonekana katika vikao vya Chadema, Dk Slaa amekuwa haonekani Katika mkutano wa leo na waandishi wa habari, Dk Slaa alieleza kwamba hakuwa likizo  kama ilivyokuwa inadaiwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe .
“Nimejitokeza leo, mimi sikuwa likizo. Mengi yamesemwa na viongozi wangu, lakini ukweli ni kwamba sikupewa likizo na yoyote, nasisitiza sina barua yoyote ya likizo.
“Kilichotokea ni kwamba niliamua kuachana na siasa tangu tarehe 28/7 majira ya saa 3 usiku, baada ya kuona yanayofanyika ndani ya chama changu na sikukubaliana nayo,” alisema Dk Slaa.
Akisimulia kadhia nzima, Dk Slaa alisema baada ya Lowassa kukatwa kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia CCM mjini Dodoma, alipigiwa simu na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima aliyemwita kuwa mshenga wa Lowassa, akimuarifu hatua hiyo ya kukatwa Lowassa ni mtaji kwa Chadema.
Hata hivyo alisema kwamba tangu awali aliweka msimamo kwamba  Lowassa kwanza atangaze kutoka ndani ya CCM, baada ya kutangaza hilo atangaze pia ni chama gani anakwenda, halafu tatu atumie nafasi hiyo kujisafisha na tuhuma zake anazoshutumiwa.
Alisema kinyume na msimamo aliouweka, Lowassa hakutangaza kujitoa CCM na kutangaza anakwenda chama gani kwa wakati huo, lakini pia hakujisafisha hadi alipokuwa katika kikao cha utambulisho Chadema ndipo alipozungumzia suala la Richmond .
Alisema mbali ya msimamo huo, aliweka msimamo mwingine wa kutaka kujua, Lowassa anakwenda Chadema akiwa ni mali au mzigo.
Alisema kutokana na swali hilo, alijibiwa kwamba Lowassa angekwenda Chadema na wabunge 50 waliokuwa wakimaliza muda wao, wenyeviti wa CCM wa mikoa 22, wenyeviti wa CCM wa wilaya 88.
Hata hivyo hiyo haikufanyika na katika vuta nikuvute kwenye kikao aliamua kujiuzuru….
“Tulirejea tena katika kikao kuanzia saa 9 jioni hadi saa 12.30, tukapumzika, lakini hatukuelewana. Wakaunda kamati ndogo ya kuzungumza na mimi na kunishauri, lakini nilikataa. Pale pale niliandika barua ya kujiuzulu nikampa Mwenyekiti wa kikao, Profesa Safari (Abdalah) lakini aliichana pale pale.
“Sikuridhika na hatua hiyo niliandika barua nyingine na kumkabidhi Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar ambaye alinijibu kwamba Dk Slaa unajisumbua bure haya mambo yamepangwa. Hata hivyo, kesho yake niliandika barua rasmi ya kujizulu,”.
Akizungumzia nini kilifuata baada ya Lowassa kupokelewa Chadema; alisema alikwenda kama mzigo na si mali kwani yeye na wafuasi wake ni watu ambao ama walikataliwa na wananchi katika kura za maoni, au ni ambao wamekuwa wakituhumiwa katika masuala ya ufisadi na hawawezi kukubalika ndani ya jamii.
Kuhusu Richmond, Dk. Slaa alisema bado anaamini kuwa Lowassa hawezi kukwepa kashfa hiyo na alionesha na kusoma vielelezo na barua mbalimbali alizosema zinadhihirisha Lowassa kuwa mpangaji mkuu wa mpango wa ufisadi wa Richmond na kwamba kupokelewa na Chadema kumekifanya chama hicho kupoteza nguvu ya hoja ya kupambana na ufisadi, hoja aliyosema ilikuwa silaha pekee kwa Chadema.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo