Rais Kikwete: Utawala wangu umefanya mambo mengi makubwa ya maendeleo

Rais Jakaya Kikwete amesema tangu achukue kijiti cha uongozi mwaka 2005 hadi leo, utawala wake umefanya mambo mengi makubwa ya maendeleo. 

Amesisitiza kuwa watu wanaobeza maendeleo hayo, waendelee kusema kwa kujifurahisha, ila wakumbuke kuwa na mipaka ya kauli zao, kwani haki ya maoni au mawazo ni lazima iende sambamba na wajibu.
Alibainisha hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, waliomwalika kuzungumza nao, ikiwa pia ni sehemu ya kumuaga akielekea kumaliza muda wake wa utawala unaotarajiwa kufikia ukingoni baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
“Tena tumewaacha watu wanatumia haki yao ya kutoa maoni au mawazo yao, na wengine sasa ndio wanaomwaga radhi, uhuru wa habari nao upo, ila wakati mwingine unaleta shida, na serikali ina wajibu wa kusema hapana, kwa kuwa kila kitu kina mipaka yake,” Rais Kikwete.
Aliongeza, “Mtu akisema Kikwete nchi imekushinda, mwache aseme wee kwa kujifurahisha, nchi haijanishinda, hapa ilipo leo ni tofauti na ilivyokuwa mwaka 2005, nilipoichukua, lakini ni lazima tuwe na mipaka ya kusema”.
Uamuzi mgumu Akizungumzia mafanikio ya utawala wake, Rais Kikwete alisema kupitia uongozi wake amefanya uamuzi mgumu wa maendeleo, ambayo mara nyingi si rahisi kwa viongozi kuyafanya hasa ya kuamini utendaji kazi wa wanawake.
“Ni katika utawala wangu nimefanya mambo magumu ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza uwiano wa jinsia kwenye ngazi ya maamuzi jambo ambalo mara nyingi wanaume hawawaamini wanawake, ila ni kupitia uongozi wangu nimeteua zaidi ya majaji 44, wanawake kwenye ngazi ya maamuzi”, alisema Rais Kikwete.
Gesi na umasikini Aliongeza kuwa katika utawala wake kiwango cha umasikini nacho kimepungua kwa asilimia 28, na kwamba mategemeo yake ni kuwa huenda yeye akawa Rais wa mwisho kuongoza Tanzania yenye umasikini, kwani fedha za gesi zilizo mbioni kuja zitamsaidia Rais ajaye kuongoza.
“Pengine nikawa rais wa mwisho kuongoza nchi masikini kwa sababu mapesa ya gesi tunayotazamia kuja yatamsaidia Rais ajaye na nchi itaondokana na umasikini na fedha hizo matokeo yake yataanza kuonekana mwaka 2020”, alisema Rais Kikwete.
Alisisitiza kuwa, ni lazima fedha hizo za gesi ziwekwe akiba, kwani rasilimali gesi ni kitu kinachokwisha, hivyo vizazi vijavyo na wao wana haki ya kuja kukuta matunda ya gesi hiyo.
Suala la albino Akizungumzia uhalifu dhidi ya walemavu wa ngozi (albino), Rais Kikwete alisema vitendo vya uvunjifu wa haki ya kuishi kwa kundi hilo ni jambo lisilovumilika, kwani albino nao wana haki ya kuishi kama binadamu wengine.
Tatizo hapa ni ushirikina, imani hii imewafanya watu wanaua wenzao kisa eti utajiri, jambo ambalo halina ukweli wowote, ila tunaendelea kupambana nalo kwa kuwaelimisha watu na wanaopatikana na hatia vyombo vya sheria vinachukua mkondo wake”, Rais Kikwete.
Alisema tangu aingie madarakani hajaidhinisha hukumu ya kunyongwa kwa wenye hukumu hizo, kwani hukumu hiyo sio nzuri na kuwa muda uliobaki anaamini hataidhinisha hukumu hizo.
“Nasoma hukumu za kunyonga wakosaji wakati mwingine unasoma hukumu mtu kaua wazazi wake kwa kuwakatakata mapanga vipande na kuvitumbukiza chooni kimoja baada ya kingine, unakasirika wee, unasema ngoja nilale kesho nitapata jibu jingine, ila ukweli adhabu ya kifo sio nzuri, ndio maana tunawafunga kifungo cha maisha,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa, mauaji ya albino ni tatizo linalotia aibu nchi na kuifadhaisha, ila serikali itaendelea na juhudi za kuelimisha jamii kuondokana na dhana potofu ya kwamba viungo vya albino vinaongeza utajiri.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo