Nyama ya Punda kugeuka dili huko Dodoma, Serikali yaonesha ukali wake

Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefungia na kukitoza faini ya Sh milioni 200 kiwanda cha kusindika nyama ya punda cha Huwacheng kilichopo katika Kata ya Kizota, mjini hapa.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa na raia wa China, kimefungiwa kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni ufanyaji wa biashara kinyume na utamaduni wa Watanzania pamoja na mazingira yasiyoridhisha kiwandani hapo.
Ofisa Mwandamizi wa NEMC, Madoshi Makene, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa watatoa barua itakayokuwa na faini ya kiasi kisichopungua Sh milioni 200 kwa kuwa wamekiuka sheria nyingi ambapo aliwataka kuacha shughuli zote za uchinjaji wa punda.
“Wamiliki wa kiwanda hiki wamekiuka sheria nyingi za nchi. Wanatakiwa wafuate sheria za nchi. Ilikuwa wajue, je inaruhusu kuchinja punda? Wanatakiwa watafute mtaalamu ambaye atasema kama kuchinja punda kisheria inakubalika na jamii au la,” Dk Madoshi.
Naye mwanasheria kutoka Baraza hilo, Manchari Heche akizungumzia kufungwa kwa kiwanda hicho, alisema kuwa uwekezaji uliofanywa na raia hao kutoka nchini China umekiuka taratibu ambapo alidai kuwa nyaraka walizonazo haziruhusu kuchinja punda.
“Tumekifunga kiwanda hiki kutokana na kuwa na mazingira mabovu, kwanza hayaruhusu kuchinja punda, binadamu wanaishi humuhumu ndani ya kiwanda na eneo ni chafu, maji na damu zimezagaa. Hata nyaraka walizotuonesha hazieleweki na hazijaonesha kuwa kiwanda hiki ni kwa ajili ya matumizi gani lakini wenyewe wanachinja punda,” alisema mwanasheria huyo.
Aliongeza kuwa nchi ya Tanzania haina uwezo wa kuwalisha raia wa China zaidi ya bilioni 2 kwa kutegemea nyama ya punda kutoka mkoani Dodoma.
“Kwanza punda ni wanyama ambao hawapatikani kwa wingi hivyo tunaamuru kiwanda kufungwa na waliopo waachiwe huru na mitambo ya kiwanda hiki izimwe,”alisema Heche.
Maofisa hao wa NEMC walisema mbali na kufungia kiwanda hicho wataendelea kufanya ukaguzi endelevu utakaowezesha kufichua viwanda vingine vya aina hiyo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo