Mbunge CCM huko Lindi ahamia CUF

Mbunge wa Viti Maalumu CCM Mkoa wa Lindi, Riziki Rurida amekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF). 

Rurida alikabidhiwa kadi ya CUF na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika Mchinga, Lindi Vijijini. 

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, ilisema katika mkutano huo wanachama 650 wa Mbunge huyo ambaye ametumikia wadhifa huo kwa vipindi viwili, alisema anajisikia mwenye furaha baada ya kukabidhiwa kadi na kuwa mwanachama wa CUF. 

Rurida alikuwa ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliowania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Mchinga na kuangushwa na mbunge wa sasa, Said Mtanda akiwa wa pili na kulalamika kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na mizengwe.

Akimkaribisha CUF, Maalim Seif alisema wimbi la mabadiliko nchini linaloongozwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni kubwa hakuna atakayeweza kulizuia. “Hili wimbi ni kubwa, mnasikia vigogo wa CCM wanaendelea kuporomoka na kujiunga na wapinzani, atakayejaribu kupingana na wimbi hili atapasuka kifua,” alisema Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. 

Maalim Seif alikemea tabia ya baadhi ya viongozi na askari polisi kuwazuia wananchi wasitumie haki yao ya kidemokrasia ikiwamo kufanya maandamano na kuwahimiza wafuate sheria na wajiepushe na uvunjifu wa haki za binadamu. 

“Polisi nchini kote fuateni sheria, hamtakiwi kuingia kwenye siasa, lakini kama kuna kiongozi wa jeshi anajiona ni CCM kuliko hao CCM wenyewe, basi avue magwanda aje tupambane kwenye majukwaa ya siasa,” alisema. 

Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwan alisema wananchi wa mikoa ya Kusini wana kila sababu ya kuikimbia CCM kutokana na sera zake mbovu ambazo hazijawasaidia wala kuwapa matumaini yoyote. 


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo