Hali ya sintofahamu imeendelea kujitokeza katika jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, ambapo licha kufanya marudio ya uchaguzi wa kura za maoni kwa mara ya tatu bado wagombea 11 wa CCM kati ya 12 waliojitokeza kugombea katika jimbo hilo,wamegoma kusaini matokeo wakimtuhumu mgombea aliyetangazwa kuwa mshindi Bwana. Edwin Ngonyani kwamba amewanunua viongozi wa wilaya pamoja na baadhi ya wananchi ambao sio wanachama wa CCM kupinga kura na kutekeleza adhma yao.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Songea mkoani Ruvuma, wagombea hawa watano kati ya 12 waliojitokeza kugombea nafasi ya ubunge wa jimbo la namtumbo,wamesema wanalaani hujuma na fitina zinazofanywa na mgombea mwenzao Bwana.Edwin Ngonyani wakidai kwamba ametumia uwezo wake wa kifedha kuwanunua baadhi ya viongozi wa chama cha mapinduzi wa wilaya ya namtumbo na kuwarubuni baadhi ya watu ambao si wanachama wa CCM kumpigia kura.
Mbali ya malalamiko hayo,wagombea hawa wakaja na mapendekezo kadhaa likiwemo la kuwaengua baadhi ya wagombea ubunge katika mchakato huo wa kura za maoni.
Hata hivyo mgombea ubunge anayetuhumiwa na wenzake Bwana.Edwin Ngonyani alipopigiwa simu yake ya mkononi amesema huo ni upuuzi na hahusiki kwa lolote huku mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya namtumbo Bwana Benjamin Nindi naye akijitetea kwamba yupo kwenye pikipiki hivyo hawezi kuongea.