Helikopta ya Nyalandu kwenye kampeni za CCM ni balaa

Na Joachim Mushi, Singida
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini anayeomba kuchaguliwa tena, Lazaro Nyalandu amenogesha kampeni za mgombea mwenza wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Bi. Samia Suluhu katika mikutano yake inayoendelea ya kuinadi ilani ya CCM.

Nyalandu ambaye jana alishuka kwa helkopta ya kukodi Jimboni kwake ikiwa ni muda mfupi baada ya mkutano wa kampeni kuanza alivuta hisia za wanaCCM na wananchi katika mkutano huo. Kama hiyo haitoshi mgombea huyo wa ubunge alitumia helkopta hiyo kwenye mikutano ya kampeni za mgombea mwenza ya Jimbo la Iramba Magharibi.

Akihutubia mkutano wa kampeni katika Kata ya Kengege, Jimbo la Iramba Magharibi mkoani Singida, Bi. Suluhu aliwaomba wananchi kuipigia kura CCM kwani ndani ya ilani yake imepanga kufanya mambo mazuri kwa maendeleo ya mkoa huo. Alisema endapo watachanguliwa watajenga kiwanda kikubwa cha kusafishia mafuta ya alizeti jambo ambalo litaongeza thamani ya mazao kwa wakulima wa eneo hilo.

Aliongeza kuwa mbali na kiwanda hicho kikubwa kuwanufaisha wakulima pia kitatoa nafasi za ajira kwa vijana ambapo jumla ya wafanyakazi 600 watapata ajira ndani ya kiwanda hicho, alisema baada ya Serikali ya awamu ya nne kujenga shule za Sekondari za kata za kutosha na maabara ilani mpya ya CCM imepanga kushughulikia suala la vifaa vya maabara hizo ili ziweze kutumika kwa ufasaha.

Bi. Suluhu alisema Mkoani Singida imepanga kujenga hospitali kubwa ya rufaa ambayo itakuwa ikitoa huduma katika mkoa huo na mikoa ya jirani, pamoja na ujenzi wa barabara ya Ndago.

Aidha akihutubia katika Mkutano mwingine Wilaya ya Ikungi aliahidi kufanya jitihada za ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Ikungi ili kusongeza huduma kubwa za afya kwa wanaIkungi, pamoja na kuvipatia umeme vijiji ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo kupitia mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya pili.

Aliongeza kuwa licha ya maeneo ya mikoa ya singida kukabiliwa na tishio la ukame aliwahakikishia hakuna raia atakayekufa njaa katika maeneo hayo. “…Serikali imejipanga na ghala la kuhifadhi chakula lina akiba ya kutosha, hivyo niwahakikishie hakuna mwanakijiji ambae atakufa kwa njaa.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Kampeni Taifa, Mwigulu Nchemba ambaye pia ni mgombea wa ubunge Jimbo la Iramba Magharibi akizungumza jimboni hapo alisema ilani ya CCM imepanga kutekeleza miradi ya maji katika Vijiji vya Mgundu, Kinampanda, Makunda pamoja na vijiji vingine vinavyokabiliwa na kero ya maji.

Alisema baadha ya mradi wa ujenzi wa shule za Sekondari za kata kufanikiwa serikali itakayoundwa na CCM imepanga kusimamia ujenzi wa mabweni ili kuwanusuru watoto wanaotembea umbali urefu kwenda shuleni pamoja huku wasichana wakikabiliwa na changamoto za kubebeshwa mimba na kukatishwa masomo yao.

Mwingulu aliwataka wananchi kutochagua vyama vingine kwani havina hoja za msingi na vingine vinaazima hadi wagombea ili viweze kuwasimamisha. Bi. Suluhu anaendelea na ziara yake ambapo sasa anaelekea Mkoa wa Dodoma akiinadi ilani ya CCM.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo