Haki za binadamu wawakaba koo wagombea wenye kashfa

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeitaka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kutoa orodha ya viongozi wa umma wanaogombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu, ambao walishahojiwa na kuwekwa hatiani kutokana na maadili yao.

Chombo hicho kimetakiwa kutowafumbia macho viongozi wanaowania nyadhifa mbalimbali ambao walishindwa kuonesha kiwango cha juu cha maadili wakati wa uongozi wao au wakati wakiwa katika nyadhifa walizowahi kushika.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo Bisimba alisema hayo jana Dar es Salaam, wakati akizungumzia maadili ya viongozi wa umma wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeshabariki kuanza rasmi kwa kampeni za kuwania nafasi hizo.

“Katika kipindi hiki tumeshuhudia vyama vya siasa vikipitisha viongozi kuwania nyadhifa mbalimbali na katika michakato mbalimbali ya vyama na kuonesha viashiria vya kutoheshimu misingi ya maadili,” alisema Dk Bisimba.

Alisema baadhi ya walioteuliwa wameshahusishwa, kutajwa na kushitakiwa katika vyombo vya kisheria na vya kikatiba kwa tuhuma za utovu wa maadili.

Alizitaja kashfa hizo kuwa ni rushwa, matumizi mabaya ya ofisi za umma na kutowajibika, vitendo ambavyo ni kinyume na misingi ya Katiba, sheria na ahadi ya uadilifu ambayo kiongozi wa umma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 kifungu cha 6.

Dk Bisimba alisema sheria hiyo inamtaka kiongozi wa umma kuwa mtu atakayekuwa na kiwango cha juu cha maadili kadri iwezekanavyo, ili wananchi kuwa na imani na kutotiliwa shaka katika uadilifu wake.

Ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutopitisha majina ya wagombea waliopendekezwa na vyama mbalimbali, ambao walishatuhumiwa au kushitakiwa kwa kashfa za rushwa, kujilimbikizia mali na matumizi mabaya ya ofisi za umma.

Kwa misingi hiyo, Dk Bisimba pia ameisisitiza sekretarieti iweke wazi majina ya viongozi wa umma ambao hawajatoa taarifa kuhusu mali walizonazo kwa mujibu wa sheria.

Aidha, ameitaka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kwa kuzingatia Sheria za Kupambana na Kudhibiti Rushwa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi, kuweka na kusimamia mkakati utakaodhibiti mianya ya rushwa na matumizi yasiyo halali ya fedha katika kampeni hizo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo