Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU) mkoani Iringa, wamelalamika kutokupewa fedha za kujikimu na za mafunzo kwa vitendo.
Wanafunzi hao ambao hawakutaka majina yao kuandikwa, walisema wamekuwa wakifuatilia fedha hizo kwa muda mrefu kwenye uongozi wa chuo pamoja na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) bila ya mafanikio.
Walisema wenzao waliokuwa wanadai fedha hizo walikuwa wengi, lakini ni wanafunzi wachache waliofanikishwa kutatuliwa tatizo lao.
“Tulikuwa wengi tunaodai fedha hizo, lakini ni wanafunzi wawili tu ambao walipewa, sisi wengine bado tunahangaika hatujui tumfuate nani kwa kuwa HESLB tumeshaenda na hakuna kitu,” alisema mmoja wao.
Wanasema kuwa uongozi wa chuo umekuwa ukiwapa majibu kuwa HESLB hakuna fedha, hivyo wanapaswa kuwa wavumilivu.
Waziri wa Mikopo wa Wanafuzi Rucu, Walter Raymond, alithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo.
Alisema kuna wanafunzi wa mwaka wa tatu wanaosomea Ualimu hawajalipwa fedha za utafiti, mwaka wa tatu waliosomea Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), wanafunzi wa mwaka wanne waliomaliza Sheria, mwaka wa tatu waliomaliza Sayansi ya Kompyuta pamoja mwaka wa tatu waliomaliza Sayansi ya Mazingira.
Afisa mikopo wa chuo hicho, Chesco Mwalongo, alipotafutwa, simu yake iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu.
Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, alisema bodi ilishakatatua tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa chuo hicho muda mrefu.
Alisema kama kuna mwanafunzi ambaye bado ana tatizo la mikopo afike katika ofisi za bodi na kuwaona maofisa na watamsadia.
Alisema matatizo ya mikopo kwa wanafunzi yanatatuliwa na bodi na siyo sahihi wanafunzi kukimbilia kwenye vyombo vya habari.
