Baba atuhumiwa kumuua mtoto wake, kisa mahari

Mkazi wa Kijiji cha Imwelo, Kata ya Buseresere, wilayani Chato mkoani Geita, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma ya kumuua mtoto wake, Pole Faida (26) kwa kushirikiana na kaka yake.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Buselesele, Daud Ruhangija alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Agosti 7 saa tano usiku nyumbani kwa mtuhumiwa baada ya kutokea malumbano kati ya baba na mtoto wake huyo.

Ruhangija alisema malumbano hayo yalitokana na mtoto huyo kumuomba baba yake kumuozesha mke, ombi lililopingwa na kaka wa marehemu.

Alisema baada ya ombi hilo kukataliwa na kaka yake, kulitokea mabishano ya familia hatua iliyosababisha Pole kuhoji sababu za msingi za kuwekewa pingamizi la kuoa, ilhali kaka yake tayari ameozeshwa tena kwa kuuza sehemu ya ardhi.

“Wakati tunamhoji baba wa marehemu kabla ya kupelekwa polisi, alikiri kuwapo mzozo uliosababisha ugomvi baina yao,” alisema Ruhangija na kumnukuu mtuhumiwa:

“Ni kweli kijana amekufa baada ya ugomvi wa muda mfupi hapa nyumbani, kikubwa ni mzozo uliotokana na mtoto kunitaka nimuozeshe kwa nguvu.”

Mtendaji huyo alisema mtuhumiwa alikiri kuwa baada ya Pole kufariki, alisaidiana na kaka yake kubeba maiti na kuipeleka kwenye mti wa mwembe na kuuvisha kamba shingoni kisha kuuning’iniza ili kuficha ushahidi.

Hata hivyo, Ruhangija alisema baada ya kuzungumza na mke wa mtuhumiwa,  aliwaeleza kuwa kabla ya kifo hicho mtoto alimtaka baba yake kuuza kipande cha shamba ili amuozeshe kama alivyofanya kwa kaka yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba upelelezi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo