Tume ya uchaguzi yaongeza siku uandikishaji kwenye daftari la wapiga kura DSM

Tume ya taifa ya uchaguzi NEC imeongeza siku nne kwa zoezi la uandikishaji daftari la kudumu la wapiga kura mkoa wa Dar es Salaam huku idara ya uhamiaji ikibaini kuwepo kwa raia wa kigeni zaidi ya 2000 ambao walijaribu kujiandikisha na baadhi yao walishapata vitambulisho vya kupiga kura.

Mwenyekiti wa NEC jaji mstaafu Damian Lubuva ameyasema haya jijini Dar es Salaam ambapo amesema hatua hiyo imetokana na mwamko mkubwa wa wananchi kujitokeza kwa wingi isivyo kawaida katika vituo vya kujiandikisha na kuongeza kuwa hadi july 29 mwaka huu wameandikisha watu milioni 18,826,718 na lengo ni kuandikisha watu wasiopungua milioni ishirini na nne hivyo kwa takwimu hizi zaidi ya watu milioni nne bado hawajajiandikisha.
 
Aidha jaji Lubuva amewataka wana Dar es Salaam kutumia muda huo vizuri kwani hakuna muda mwingine utakaoongezwa kutokana na siku za kampeni kukaribia ambapo akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari ikiwemo vituo kuendelea kufunguliwa saa mbili asubuhi licha ya tume kutangaza kuwa vitafunguliwa saa moja asubuhi pamoja na tatizo la waandikishaji kuwa na kasi ndogo.
 
Zoezi hili kwa mkoa wa Dar es Salaam lilikuwa likamilike July 31 ambapo katika vituo mbalimbali vya kujiandikisha idadi ya watu bado imeendelea kuwa kubwa huku baadhi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha wakilalamikia upendeleo unaofanywa na wasimamizi ambao wamedai kuwa wanawapa watu wanaowajua kipaumbele ili hali baadhi yao wamefika kituoni hapo alfajiri kwa ajili ya kuwahi namba.
 
Katika hatua nyingine idara ya uhamiaji nchini imebaini raia wa kigeni zaidi ya 2000 waliojitokeza kujiandikisha katika daftari hilo tangu zoezi hilo lilipoanza ambapo mikoa 14 imehusika na mikoa iliyoongoza ni kagera iliyokuwa na watu 708, mara 619, tanga 348, kigoma 254 na dar es salaam ambako zoezi bado linaendelea raia wa kigeni 65 tayari wameshabainika na kuongeza kuwa wapo ambao tayari wamesharejeshwa makwao.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo