
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amekanusha kumshushia kipigo Dk. Joseph Chilongani, ambaye ni mgombea mwenzake katika mchakato wa Chama Cha mapinduzi (CCM), kupata mgombea ubunge Jimbo la Kongwa.
Awali ilidaiwa kuwa Jumatatu jioni Ndugai, alitumia fimbo kumpiga Dk. Chilongani, ambaye alipoteza fahamu kabla ya kupelekwa hospitali ya wilaya hiyo, ambako aliendelea na matibabu mpaka jana aliporuhusiwa.
Mganga Mkuu wa Wilaya, Festo Mapunda, alilieleza NIPASHE jana kuwa walimruhusu kutokana na hali yake kiafya kuwa nzuri.
Naye Naibu Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, hakuwa tayari kueleza ikiwa mpaka jana alikuwa amepokea taarifa rasmi ya tukio hilo kutoka kwa walalamikaji badala yake alisema Dk. Chilongani, jana aliendelea na kufanya kampeni kama kawaida.
Madai dhidi ya Ndugai yalielezwa na Dk. Chilongani, kuwa sababu ya mtafaruku huo ilikuwa mzozo uliyoibuka kati ya Ndugai na mgombea mwingine, Simon Ngatunga, na baadaye Ndugai kumtuhumu Dk.
Chilongani kuwa alikuwa akitumia simu yake ya kiganjani, kumrekodi video ili kusambaza mitandaoni. Hata hivyo Ndugai alisema jana kuwa miongoni mwa wagombea tisa wanaowania nafasi hiyo, baadhi wamepandikizwa kwa lengo la kufanyia fujo.
“Tangu tuanze kampeni, wagombea mapandikizi wanafanya kazi ya kunitukana na kunidhalilisha kila tunakokwenda, mmoja ananiporomoshea matuzi ikitokea nikajibu, wanakuwa wameshapanga mmoja wao wa kunirekodi ili wazidi kunidhalilisha mitandaoni,” alieleza Ndugai
Alisema tukio la Jumatatu, wakiwa kwenye mkutano wa hadhara Ngatunga, alimtukana matusi ya nguoni na kusababisha mzozo kati yao, wakati watu wakiendelea kumsihi ampuuze yule kijana huyo akagundua Dk. Chilongani akitumia simu yake kumrekodi.
“Nilishamuonya mara kadhaa aache kujifanya mwandishi wa habari, kwa kuachukua video tena akinilenga mimi tu, lakini hakusikia nilichofanya niliigonga ile simu aliyokuwa akiitumia kuchukua video,” Ndugai alisema.
“Nikaigonga nikimwambia hebu usiendelee kunichukua video na kikamera chako hicho simu ikaanguka chini, nikashangaa kuona na yeye akijiangusha chini kama wachezaji wa mpira wa miguu, ambao hujiangusha kwa lengo la kusingizia wamefanyiwa fujo ili wenzao wapewe kadi nyekundu.”
Kwa mujibu wa Ndugai, hakumpiga Dk. Chilongani wala hakujaribu kumpiga Ngatunga.
CHANZO: NIPASHE