Mkoani Dodoma, Shirika la umeme nchini (TANESCO) limekiri kuwepo kwa mgao mkali wa umeme katika mkoa huo, kulikosababishwa na kuendelea kwa matengenezo ya njia kubwa za umeme katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma.
Akizungumza na waandiishi wa habari mjini Dodoma, Afisa Uhusiano wa TANESCO Dodoma Bw. Innocent Lupenza amesema marekebisho hayo yameanza sasa baada ya kukamilika kwa vikao vya bunge na vya chama cha mapinduzi, na akakiri kuwa kuchelewa kutolewa kwa ratiba ya mgao, ili wateja wao waweze kufahamu ni muda gani watakuwa na umeme.
Baadhi ya wateja wa shirika hilo wameilaumu TANESCO kwa kufanya marekebisho bila ya kutoa ratiba ya mgao na hivyo kuwasababishia hasara, kama mmoja wa wamiliki wa kiwanda cha kukamua alizeti Bw. Daudi Sudaye anavyobainisha.
Kwa takriban wiki mbili sasa wateja wa shirika hilo la umeme kwa mkoa wa Dodoma wamekuwa katika mgao mkali wa umeme, huku watendaji wa shirika hilo wakijitetea kutoa taarifa kwa umma juu ya kufanya marekebisho, lakini bila ya kutoa ratiba ya mgao wa umeme, itakayoonyesha ni kwa kipindi gani marekebisho hayo yataendeshwa.
