Familia ya Luciano Chole, mkewe na mwanawe, wameuawa kinyama baada ya vijana watatu kuwakamata na kuwapiga mapanga na marungu na miili yao kuiteketeza kwa moto Sumbawanga.
Hukumu ya kesi hiyo imetolewa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Sumbawanga, Mwakipombe Sambo ambapo ushahidi uliotolewa Mahakamani ulieleza kuwa familia hiyo ilitendewa unyama huo Aprili 17, 2011 katika Kijiji cha Miombo, Kata ya Mtenga wilayani Nkasi.
Kwa mujibu wa ushahidi washitakiwa wa mauaji hayo, Shija Ndigila, Deus Kizipe naGalus Antony, wanadaiwa walifika nyumbani kwa Chole siku ya tukio wakiwa na ujumbe kwa mtoto wake, Jailos Silvanus.
Ilidaiwa kuwa vijana hao watatu, walimweleza Chole na mkewe kuwa kijana wao, Jailosalikuwa akihitajika kwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho.
Baada ya kukubaliwa kuondoka na Jailos, wazazi hao waliamua kufuata vijana hao kwa kificho na kisha wakishuhudia kijana wao akishambuliwa kwa marungu na kucharangwa kwa mapanga mpaka akafa.
Imedaiwa kuwa baada ya kuuawa kwa Jailos, wauaji hao walibaini kuwa wazazi wa kijana huyo walikuwa wakishuhudia, ndipo walipowavamia na kuwaua kikatili kwa kuwacharanga kwa mapanga.
Wauaji hao imedaiwa waliamua kukusanya miili ya marehemu na kuifunika kwa nyasi miili yao na kuichoma moto. Mbali na kuteketeza miili hiyo, ilidaiwa kuwa wauaji hao baada ya kumaliza ukatili huo, walikwenda nyumbani kwa wanafamilia hao na kuiteketeza nyumba yao kwa moto kisha wakatokomea kusikojulikana.
Baada ya kusikiliza kesi hiyo, Jaji Sambo aliwahukumu washitakiwa hao kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kuua watu watatu wa familia moja.