Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amepita bila kupingwa katika mchakato wa kura ya maoni ya ubunge wa jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro, baada ya kuvuna kura 269.
Licha ya kupita kwa kishindo, wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi huo, walimpigia Mbowe kura tano za kumkataa.
Akitangaza matokeo, Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini na Mbunge wa Karatu, Mchungaji, Israel Natse alisema: ” Mbowe aliyekuwa mgombea pekee wa nafasi ya ubunge, alipigiwa kura za ndiyo 269 sawa na asilimia 98.2, lakini pia alipigiwa kura tano za hapana na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Kura ya Maoni.”
Akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa mkutano huo, kuhusu haki ya kikatiba ya wajumbe wa mkutano huo kupiga kura ya hapana; Mchungaji Natse alisema kuwa kura za kumkataa zilitokana na kukua kwa demokrasia ndani ya chama hicho kinachojiandaa kushika dola baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Katika uchaguzi huo uliofanyika katika mji mdogo wa Bomang’ombe, wajumbe halali waliopaswa kushiriki zoezi hilo walikuwa 274 kutoka Kata zote za Wilaya hiyo.
Hata hivyo; akizungumza muda mfupi baada ya kutangazwa matokeo hayo, Mbowe alisema,”Nawashukuru sana wajumbe kwa kuniamini na kunipa heshima ya kuendelea kutetea ubunge wa Hai na pia kuendeleza mapambano dhidi ya utawala wa CCM. Nawahakikishia kwamba nitashinda tena kwa kishindo na moto watauona mwaka huu.”
Mbowe alisema sababu ya yeye kuendelea kupigania ukombozi wa nchi kutoka mikononi mwa CCM ambayo imewagawa Watanzania katika makundi ya walionacho na wasionacho, hakuwezi kumfanya asiwaze juu ya ukombozi wa fikra na maendeleo ya kweli dhidi ya umma wa Watanzania.