Mawaziri wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona jana wamekata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga hukumu iliyotolewa dhidi yao ya kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya Shilingi milioni tano.
Hukumu hiyo ilitolewa Julai 6 mwaka huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kukutwa na hatia ya mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.
Baada ya hukumu hiyo, jana Wakili wa Serikali, Timothy Vitalis alisema Mahakamani hapo kuwa waliwasilisha maombi ya kukata rufaa wakitaja upungufu wa aina tatu kwenye mwenendo wa kesi iliyopita kwamba hati ya mashtaka haikuwa sahihi.
Alitaja eneo la pili lililosababisha kukata rufaa kuwa ni ushahidi wa Jamhuri haukuwa na uzito wa kuwatia hatiani na pia adhabu iliyotolewa ilikuwa ni kubwa.
Katika rufaa hiyo, Jaji wa Mahakama hiyo, Salvatory Bongole aliieleza Mahakama kuwa hataweza kuendelea na kesi hiyo kwa sababu mmoja wa waliokata rufaa anafahamiana naye.
Kesi hiyo itasikilizwa Julai 31 mwaka huu kwa sababu anayetarajia kuiendesha atatoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza mwaka 2008 wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya Uingereza.