Kumbe Bulaya aliahidiwa uwaziri au ukuu wa wilaya ili asihame CCM

Mbunge wa Viti Maalum alihama juzi CCM na kujiunga Chadema, Ester Bulayaamesema licha ya kuahidiwa vyeo vingi ukiwamo uwaziri na ukuu wa wilaya ili asihame CCM, aliamua kuviacha ili aweze kuwasaidia Watanzania wa chini ambao wameonewa na serikali ya chama hicho kwa miaka 50 iliyopita.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyikia katika Viwanja vya Stendi ya zamani mjini Bunda jana, Bulaya alisema wakati chama chake cha zamani kilipogundua mikakati yake ya kuhamia Chadema, makada wake walimwendea wakimsihi asitoke, bali abakie ili apatiwe ukuu wa wilaya au uwaziri.
Bulaya aliyeambatana na Mbunge wa Kahama, James Lembeli ambaye pia alijiunga na Chadema juzi, alisema baada ya kutafakari kwa muda mrefu uhalisia wa maisha ya Watanzania hasa wa vijijini na jinsi ambavyo Serikali ya CCM imekuwa ikiwatendea, aliamua kuachana na ahadi hizo na kujiunga na Chadema kwa kuwa inalenga kuwakomboa Watanzania.
“Ngojeni niwaambie, niliahidiwa ukuu wa wilaya na uwaziri ilimradi tu nisihame CCM. Lakini nikaona yote hayo ni upuuzi, bali cha muhimu ni kuwakomboa Watanzania, nikaachana nayo yote nikaja Chadema,” alisema.
Bulaya aliyejigamba kukulia na kufanya kazi ndani ya CCM, alisema chama hicho hakina sera zozote za kuwakomboa Watanzania badala yake kuna za kuwanufaisha wachache, jambo ambali yeye na Lembeli hawakulitaka.
Bulaya alitangaza azma yake ya kugombea ubunge katika Jimbo la Bunda Mjini, akisema tayari ameshajaza fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi hiyo.
Niwaambie tu kwamba nimeshajaza fomu na kuirejesha na kesho (leo) nitashiriki kura za maoni. Inshallaah Mungu akinisimamisha nitagombea nafasi hiyo na nina uhakika wa kushinda,” Bulaya.
Lembeli aliwataka wakazi wa jimbo hilo kutoipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao, badala yake waichague Chadema kwa nafasi zote bila kumsahau Bulaya kwa ubunge kwa kuwa ni mtu mwadilifu.
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee akihutubia mkutano huo aliwataka Watanzania wakubali kula fedha wanazogawa na makada wa CCM ili wachaguliwe kwa nafasi mbalimbali za urais, ubunge na udiwani lakini kura zote waipatie Chadema.
chanzo:mwananchi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo