Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa Mkoa wa Dar es Salaam, unaendelea pamoja na kujitokeza kasoro kadhaa, ikiwa na pamoja na baadhi ya watu kutumia mbinu mbalimbali ili kukwepa foleni.
Katika Kituo cha Bwawani Shule, Mtoni Kijichi, wanawake wawili waliojifanya wajawazito walibainika kufanya udanganyifu huo huku mmoja akiwa tayari amejiandikisha.
Hata hivyo, mmoja wa majirani ambaye anawafahamu, alidokeza kuwa anawafahamu wasichana hao na hawakuwa na wajawazito.
Mmoja alikuwa amekwishajiandikisha na aliwahi kuondoka mapema kabla ya mwenzake aliyekuja kwa staili hiyo na kushtukiwa.
Baada ya mzozo huo, aliondoka taratibu eneo la tukio ndipo baadhi ya watu walipoanza kumkimbiza kubaini iwapo ni mjauzito au la, msichana huyo alitoa makaratasi aliyokuwa ameyafunga tumboni kama ujauzito na kuyatupa, huku akikimbia na kutokomea katika vichochoro vya Mitaa ya Mtoni Kijichi.
Mmoja wa wasimamizi wa kituo hicho, alisema kuwa hawana kawaida ya kuwakagua isipokuwa wanachoangalia ni hali za watu wakiwamo wajawazito, walemavu, wazee na wenye watoto wachanga.
Katika Vituo vingine baadhi ya wananchi walilazimika kuzipiga kavukavu kutokana na wengine kutaka kuwapita wenzao waliofika vituoni mapema.