WAKAZI wa Mtaa wa Sechelela Kata ya Tambukareli Chadulu (A) Dodoma wanaotumia dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV), wametakiwa kuepuka matumizi ya unywaji wa pombe, uvutaji wa sigara na ngono uzembe.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sechelela, Robarnt Pangaselo, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya wanafunzi hao kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa huo.
Alisema utumiaji wa dawa hizo na unywaji wa pombe, ngono zembe pamoja na uvutaji wa sigara unachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza nguvu za dawa hivyo kuwataka wakazi wa eneo hilo wanaojihusisha na unywaji wa pombe hasa kwa wale wanaotumia dawa hizo kujiepusha.
“Changamoto tunayokubaliana nayo ni matumizi sahihi ya dawa za ARV kwani kuna wale ambao wamekuwa wakitumia dawa huku wakiwa wanakunywa pombe, wanavuta sigara pamoja na ngono zembe, niwaombe wakazi kuachana na jambo hili, tuendelee kuzitumia kwa kufuata masharti,” alisema
Hata hivyo akizungumza kwenye mkutano huo mwenyekiti huyo alisema kuwa katika mtaa huo wanakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa majengo ya shule ya Medeli kutokana na uchakavu uliopo hali inayosababisha hatari kwa watoto na walimu kuangukiwa na majengo ya shule hiyo.
Pangaselo alisema kwa sasa hali ya uchumi katika Kata hiyo sio nzuri kutokana na kuwa na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana hali ambayo imekuwa ikirudisha maendeleo nyuma.