Idara ya afya mkoani Tanga imewataka wagonjwa waliobainika kuwa wameathirika na virusi vya ukimwi kuendelea kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARV's kufuatia sehemu kubwa ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa huo Bombo kukiri kuacha matumizi ya dawa hizo.
Akizungumza katika uwanja wa Tangamano jijini Tanga wakati wa kufunga zoezi la upimaji afya bure, mratibu wa kudhibiti ukimwi mkoani Tanga Dr, Selemani Msangi amesema baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Bombo wamekiri kuacha matumizi ya ARV's kwa sababu ya dhana tofauti ikiwemo kushauriwa na baadhi viongozi wa madhehebu ya dini kuachana na matumizi ya dawa hizo hatua ambayo imeathiri zaidi makundi hayo.
Kwa upande wake daktari bingwa wa afya ya nchini Dr,Ally Mzige akielezea afya za watanzania, amesema asilimia 35% ya saratani zote zinazojitokeza katika mwili wa binadamu husababishwa na vyakula anavyotumia mlaji hatua ambayo imeathiri zaidi afya za wananchi.
Awali akielezea dhumuni la kutoa huduma ya upimaji wa afya bure, meneja wa mfuko wa afya ya jamii nchini (NSSF) Dr,Ally Ntulia amesema lengo hasa la zoezi hilo ni kuisaidia serikali kukabiliana na magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo Sataratani na Sukari yamekuwa yakiathiri zaidi afya za watanzania.