Raia watatu wa Ugiriki na Mtanzania mmoja wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kughushi muhuri wa Mkuu wa Jeshi Polisi Nchini(IGP).
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Mununila Munisi alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchaulu kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo katika tarehe na muda usiofahamika wilayani Ilala.
Alidai kwamba katika shtaka la kwanza washtakiwa hao kwa pamoja kwa nia ovu, walighushi muhuri huo wa IGP wakionyesha ni halali na umetolewa na Jeshi la Polisi la Tanzania wakati wakijua si kweli.
Shtaka la pili wanadaiwa kuwa katika tarehe zisizofahamika jijini Dar es Salaam, walighushi taarifa ya upotevu wa mali inayotolewa na jeshi hilo la polisi wakionyesha ni halali na imetolewa na polisi wakati wakijua siyo kweli.
Washtakiwa wote walikana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba ipangwe tarehe nyingine.
Hakimu aliwataka washtakiwa hao wawe na wadhamini wawili wa kuaminika na kila mmoja atasaini bondi ya Sh5 milioni .
Pia, washtakiwa hao hawaruhusiwi kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha mahakama na wametakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiria.
Washtakiwa wote walishindwa kutimiza masharti hayo na hivyo wamerudishwa rumande.