MAGARI manane Ijumaa yalichomwa huku kituo kimoja cha petroli kikiharibiwa baada ya wanafunzi wa Taasisi ya Kiteknolojia ya Gusii kufanya maandamano wakilalamikia vifo vya watu wawili katika ajali Alhamisi jioni.
Wanafunzi hao wenye ghadhabu walikabiliana na polisi kwa saa kadhaa, hali iliyokwamisha shughuli za usafiri katika barabara kuu ya Kisii-Keroka nyakati za asubuhi.
Ili kuwakabili waandamanaji hao, polisi walilazimika kufyatua risasi hewani pamoja na kuwarushia vitoa machozi katika juhudi za kuwatawanya. Umati huo ulikuwa umeongezeka maradufu, baada ya wakazi kuungana naokulalamikia mauaji hayo.
Mwanafunzi mmoja kutoka taasisi hiyo alijeruhiwa vibaya mguuni, baada ya kupigwa risasi na maafisa ambao waliitwa ili kurejesha hali ya kawaida.
Kwa wakati mmoja, maafisa hao walizidiwa nguvu na umati huo baada ya kumaliza vitoa machozi, huku mmoja wao akijeruhiwa. Umati huo uliwakabili kwa kuwarushia mawe.
Umati huo ulimshambulia afisa huyo kwa kumpiga mawe, kabla ya maafisa wenzake kufika ili kumsaidia.
Baadhi ya maafisa walilazimika kutafuta hifadhi katika afisi za Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Kahawa cha Kisii baada ya kufukuzwa na umati huo wenye ghadhabu.
Ghasia hizo zilianza Alhamisi usiku baada ya lori moja lililokuwa likisafirisha vigingi vya stima kutoka mjini Keumbu kuelekea Kisii kupoteza mwendo na kusababisha ajali iliyopepelekea vifo vya watu wawili.
Watu hao, ambao walithibitishwa kuwa wafanyikazi katika taasisi hiyo walifariki papo hapo baada ya vigingi hivyo kuwaangukia. Watu wawili zaidi walijeruhiwa ambapo walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii kwa matibabu.
Lori hilo lilikuwa limenaswa na polisi katika barabara hiyo kwa makosa ya trafiki na lilikuwa likiendeshwa na mmoja wao katika Kituo cha Polisi cha Kisii ya Kati.