Wazazi 19 wa wanafunzi walioshindwa kuripoti kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2014/2015 wamehukumiwa kifungo cha nje cha miezi mitatu kila mmoja kutokana na kosa la kushindwa kuwapeleka watoto wao shuleni.
Wazazi waliohukumiwa kifungo hiki ni wale wa kata za Mpindimbi na Lukuledi zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Masasi, Mtwara .
Aidha, wametakiwa kuripoti kwenye Mahakama ya Mwanzo ya Lisekese wilayani hapa kila baada ya wiki mbili wakati wote watakapokuwa wanatumikia adhabu yao.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Lisekese wilayani Masasi, Gloria Mkwera karani wa mahakama hiyo, Agnes Hanga alidai washitakiwa hao walitenda kosa hilo mwanzoni mwa mwaka huu waliposhindwa kutimiza wajibu wao wa kuwapeleka watoto wao shuleni huku wakijua ni wajibu wao.
