Mwenyekiti wa Kitongoji cha Suhunyi (CCM), Wilaya Siha, mkoani Kilimanjaro, Moses Kileo , amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Mjini Moshi akiwa mahututi baada ya kuvamiwa na kutekwa na kundi la watu wasiojulikana na kukata sehemu ya uume wake na kutokomea.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Godfrey Kamwela, alisema Mwenyekiti huyo alinusurika kifo baada ya watu hao kutaka kipande cha juu cha uume wake, kwa kile alichoeleza huenda kinatokana na imani za kishirikina.
“Bado tunawasaka waliohusika kumteka na kisha kumkata Moses kiungo chake kutokana na imani za kishirikina. Nimeagiza polisi kuhakikisha watu hao wanapatikana mara moja na kuchukuliwa hatua za kisheria,” Kamwela.
Alisema Mwenyekiti huyo kwa sasa hawezi kuzungumza kutokana na hali mbaya aliyokutwa nayo na kwamba Polisi wameshindwa kumhoji.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, Kileo alikumbwa na mkasa huo, Aprili 10, katika Kijiji cha Kashashi, Wilaya ya Siha.
Alidai kuwa baada ya watu hao kukamilisha zoezi hilo, walimtelekeza kando ya barabara ya Kashashi-Suhunyi, akiwa anavuja damu nyingi na baadae kutokomea na kipande hicho cha uume wake.