Mbunge wa Rufiji ambaye pia ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, juzi alichangia kuyaokoa maisha ya Amina Bakari (20), mjamzito aliyesota porini kwa saa sita akisubiri usafiri wa kumfikisha hospitali ya wilaya iliyopo Utete kwenda kujifungua.
Kabla ya msaada wa mbunge huyo aliyekuwa katika ziara jimboni kwake, Amina
alikodi pikipiki imwahishe hospitali, lakini baada ya umbali fulani, mama huyo alishindwa kuhimili mtikisiko na kuomba ashushwe kwa kuwa pia dalili za uchungu wa kujifungua zilikuwa zimeongezeka.
Dereva
wa bodaboda, Mussa Idd alisema aliridhia kumsikiliza mteja wake na
hivyo kumshusha katika eneo la Nyagolombe mpakani mwa kijiji cha Utungi
na Nyamwage, lakini kwa zaidi ya saa sita mama huyo hakupata usafiri, huku akihangaika kutokana na kushikwa na uchungu.
“Lakini tukiwa tumeshakata tamaa na kusubiri ajifungue tukiwa porini, lilitokea gari na nikasimamisha ili kuomba msaada. Kumbe lilikuwa na mbunge wetu, hakuwa na hiyana alitusaidia kumkimbiza mgonjwa hospitalini umbali wa kilometa 20…,” alisema.
Akiwa
katika ziara hiyo, Dk Rashid aliyezungukia vijiji na miradi mbalimbali,
aliwataka wananchi wa Jimbo la Rufiji kuthamini michango inayotolewa
kwa ajili ya kuimarisha afya, umeme, shule na uboreshaji wa sekta ya
mawasiliano katika wilaya ya Rufiji.
Akizungumza
juzi na watendaji wa Serikali za Mitaa ngazi ya vitongoji katika
kijiji cha Garambe, Dk Rashid alisema mambo yaliyofanyika katika wilaya
hiyo ni mengi na yenye tija kwa kila mwananchi, hivyo waiheshimu
michango hiyo kwa kuigeuza kuwa fursa za maendeleo.
Alisema
wilaya ya Rufiji inaongoza kwa kuwa na magari ya kubebea wagonjwa
kuliko nyingine hapa nchini, pia wilayani humo kumejengwa kituo cha afya
karibu kila kata pamoja na zahanati,kitu ambacho ni cha kujivunia
katika uongozi wake.
"Hadi
sasa wilaya ina magari saba ya kubebea na huenda yakaongezeka kutokana
na kuendelea kuwashawishi wafadhili wa ndani na nje ili kusaidia hilo,
pia acheni kurubuniwa na watu wachache wanaosema kuwa sijafanya
chochote hapa jimboni," alisema.
Alisema
katika kituo cha Afya Ikwiriri, kipo chumba cha upasuaji kinamaliziwa
kujengwa kwa gharama ya Sh milioni 150 ambacho kitakuwa cha kisasa na
kitasaidia wakazi wa wilaya hiyo pamoja na za jirani.