Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Udasi mwambao mwa Ziwa Tanganyika, kata ya Kabwe wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Ismail Ndomboya (42) amenusurika kuuawa na mamba kwa kupambana kijasiri na mnyama huyo kwa zaidi ya nusu saa.
Hata hivyo, licha ya kuokoa maisha yake mnyama huyo katika mapambano hayo alimng’ata na kumnyofoa mkono wake wa kushoto na kutokomea nao ziwani.
Diwani wa Kata ya Kabwe, Asante
Lugwisha akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu
alithibitisha kutokea kwa mkasa huo uliotokea juzi saa moja na nusu jioni wakati Ismail alipokuwa akioga katika Ziwa Tanganyika kijijini Kabwe .
Akisimulia mkasa huo, Diwani Lugwisha alibainisha kuwa jioni hiyo ya tukio Ismail aliamua kwenda kuoga ziwani wakati huo akiwa pekee ndipo ghafla mamba alimvamia ghfla na kumuuma mkono wake wa kulia.
“Kwa ujasiri mkubwa Ismail alipambana kufa au kupona na mnyama huyo kwa nusu saa huku akipiga yowe akiomba msaada lakini hakuna aliyejitokeza kumsaidia kwa sababu sehemu aliyokuwa akioga ilikuwa mbali na makazi ya watu,“ alieleza.
Aliendelea
kueleza kuwa hatimaye mamba aliunyofoa mkono wa kushoto wa Ismail
na kutokomea nao ziwani ndipo Ismail alipokimbia kuelekea
nyumbani kwake akiwa uchi.
“Baadaye
nilitaarifiwa kuwa Ismail ameshambuliwa na mamba wakati akioga
ndipo nilipofika nyumbani kwake, na tulijipanga tukamkimbiza katika
Hospitali Teule ya Wilaya (DDH) mjini Namanyere ambao tulifika saa
nne na nusu usiku ambako amelazwa kwa matibabu “ alieleza.
Mtaalamu
wa afya wa Hospitali ya Wilaya, ambaye alikiri kuwa si msemaji,
alikiri kupokelewa kwa mgonjwa huyo aliyejeruhiwa na mamba ambapo
aliielezea hali yake kuwa inaendelea vizuri.