Wakazi wa jijini hapa jana walizua tafrani baada ya kufunga ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa muda wakidai kupewa majibu kuhusu tatizo la upatikanaji wa umeme lililodumu kwa zaidi ya siku tano.
Tukio hilo lilitokea jana saa 4:00
asubuhi baada ya wateja hao kusubiri majibu kutoka kwa wahusika, ambao
awali walitangaziwa kuwa huduma hiyo ingeanza kupatikana juzi, lakini
mpaka jana tatizo hilo lilikuwa likiendelea.
Wakazi hao waliwafungia wafanyakazi wa
Tanesco wa kitengo cha malipo, wakisema kuwa hawafanyi kazi yoyote na
hivyo hawatakiwi kutoka nje. Hali hiyo ilidumu hadi askari wa
walipowasili na kuwashauri waondoke.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti ofisini
hapo, wateja hao walisema baada ya kukosekana kwa huduma ya luku kwa
siku tatu, jana kupitia simu zao za mkononi walipokea ujumbe
uliowataarifu kuwa huduma hiyo ingeanza kutolewa jana kwa mawakala na
katika ofisi za Tanesco, hata hivyo hali haikuwa hivyo.
Mkazi wa Mwanjelwa, Dickson Mwangunga alisema watendaji wa shirika hilo wanatoa taarifa zisizo sahihi na kusababisha usumbufu.
“Ni
vema kama wangetoa taarifa sahihi, watu tumefika hapa kwa ajili ya
kununua umeme, lakini huduma hiyo haipo. Baadhi yao wanatuambia eti hali
bado haijatengemaa, wengine wanasema tusubiri na muda unazidi kwenda,
sasa nani mkweli? ndiyo maana tumeamua kuzifunga ofisi zao watupe jibu
sahihi lini huduma hii itatengemaa,”:- Mwangunga.
Hata hivyo, sakata hilo liliokolewa na
mkuu wa upelelezi wa Wilaya ya Mbeya, Kitinkwi Mtatiro ambaye alifika
katika ofisi hizo na kuwaomba wateja hao warejee nyumbani hadi
watakapopewa taarifa ya kurejeshwa kwa huduma na uongozi wa Tanesco.
“Nawaomba
mfungue milango ya ofisi, waacheni wafanye kazi hili ni tatizo
limetokea. Hata wao hawapendi karaha hii itokee ni vema mkawa watulivu
msipende kujichukulia sheria mkononi. Jambo hili linaweza kuvuruga
amani,” :- Mtatiro.
Akizungumzia hali hiyo, meneja wa
Tanesco wa Mbeya, Amos Maganga aliwaomba wananchi kuwa watulivu kwa kuwa
tatizo hilo ni la kitaifa na mara mitambo itakaporekebishwa
watajulishwa kupitia simu zao za mkononi.
Jijini Dar es Salaam, wananchi waliendelea kulia na tatizo hilo lililodumu kwa siku tatu mfululizo.
Baadhi yao wamelalamikia hasara
wanayoipata kwa sababu ya kukosa umeme na kushindwa kufanya kazi za
uzalishaji zinazotegemea uwapo wa umeme.