
Alitoa kauli hiyo juzi wakati akifungua mafunzo elekezi kwa wakuu wapya
27 wa wilaya walioteuliwa hivi karibuni huku akiwataka kuwa na
ushirikiano na vyama vyote vya siasa.
Alisema kazi ya kuboresha daftari la wapiga kura, imeanzia Njombe na
itaendelea mikoa mingine na kuwataka viongozi hao kuhamasisha
wananchi kujitokeza kwa wingi na kukumbusha maana ya kuwa na
kitambulisho cha kura ambacho kitamwezesha kupiga kura ya maoni na
katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
“Wananchi wasipoteze fursa waone haja ya kujiandikisha na watakaokosa fursa ya kupiga kura hawataipata fursa hiyo tena.
Tunataka Watanzania wenye sifa washiriki kikamilifu kuhimiza wananchi wajiandikishe, na kupiga kura,” alisema.
Pia alisema kuna zoezi la kutoa elimu, kampeni kabla ya kura ya maoni, kutumia vizuri mamlaka ya ulinzi na amani ili mazoezi
hayo yafanyike kwa amani na utulivu.
“Wasioitakia mema nchi hii wasifanye zoezi hili likageuka la fujo na kuhujumu kampeni, wahakikishe mazoezi hayo yanafanikiwa,”
alisema. Pia Rais Kikwete alisema mwaka huu unafanyika uchaguzi mkuu akiwa ametimiza haki yake ya kikatiba.
“Nimetimiza
fursa yangu ya kikatiba, baada ya uchaguzi wa Oktoba ninakuwa mzee maarufu, tufanye uchaguzi kwa utulivu na amani ili
Watanzania wapate nafasi ya kuchagua kiongozi anayefaa,” alisema.
Alisema kuna matatizo makubwa ya mauaji ya walemavu wa ngozi na usafirishaji wa dawa za kulevya, masuala ambayo yanalitia
fedheha taifa.
“Ni jambo la aibu, kijinga na fedhehesha mtu mzima na akili yako unaamini ukipata kidole cha albino mambo yako yatakuwa
mazuri, kamati za ulinzi na usalama zikae na kuona namna gani watakabiliana na suala kama hili,” alisema.
“Lipo tatizo kubwa la dawa za kulevya ambapo vijana wanavuruga sifa nzuri ya Taifa, sasa mtu akienda nje ya nchi akijitambulisha
anatoka Tanzania anaonekana anasafirisha dawa za kulevya.
“Kiwango cha ukubwa kinatofautiana, kila mahali tatizo hili ni
kubwa sana zinatakiwa juhudi zaidi, lakini ni tatizo kubwa,” alisema.
Uteuzi wa wakuu wa wilaya Rais Kikwete alisema wakuu wa wilaya wapya waliteuliwa kutokana na kukidhi sifa na vigezo.
Pia aliwaonya wakuu wa wilaya wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kukamata wananchi na kuwaweka ndani bila sababu za
msingi, kwani baadhi yao wanajiona wana madaraka zaidi kuliko Rais wa nchi.
Alisema wakuu wa wilaya waliteuliwa kutokana na kukidhi sifa na vigezo vya madaraka yao na kuwataka wakachape kazi ili
wakidhi matarajio aliyokuwa nayo na kuwataka kutokaa maofisini kwani wanafanya kazi na jamii wanatakiwa kujua shida za watu.
“Nimewaamini naomba mkafanye kazi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa,” alisema. Aliwataka kurejea vituo vyao vya kazi na
kutekeleza kwa ufanisi mkubwa kazi zao kwa kipindi kifupi kilichobaki kabla ya kuingia uchaguzi mkuu
“Mkuu wa wilaya ndiye mwakilishi wa Rais, zamani watu walikuwa na msemo wa kula nchi kwani wanasema hapa Rais
amenikatia kipande changu sasa sio kula nchi bali kujenga nchi,” alifafanua.
Akizungumzia ujenzi wa maabara alisema kuna wilaya zimekamilisha ujenzi, lakini aliongeza miezi sita inaisha Juni kila mmoja
ajue ujenzi umefikia hatua gani na kusimamia.