MSAKO WA WAGANGA WA JADI WAZIDI KUIBUA MAZITO, ANGALIA VIFAA WALIVYOKAMATWA NAVYO

Na Nathaniel Limu, Singida
JESHI la polisi mkoa wa Singida, limetangaza vita dhidi ya waganga wa kienyeji wasiokuwa na vibali ambao wanajihusisha na kutoa ramli chonganishi.  Jeshi hilo limeanzisha msako mkali kwa waganga hao na kufanikiwa kukamata wanane katika kata moja ya Minga katika manispaa ya Singida.
Akitoa taarifa ya msako huo ulioanza machi 16 mwaka huu saa sita mchana, Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Singida, Simon Haule,alitajwa waganga hao waliokamatwa kuwa ni Mwajuma Juma (54),Rasdhid Mbwana (44),    Mariamu Joseph (35),Moshi Hassan (57),Jumanne Ramadhani (75),Mariamu Jackson (40),Mohamed Sadick (56) na Mawafutari Juma (39).
Alisema waganga hao wamekamatwa wakiwa na nyara za serikali ambazo wanazitumia katika shughuli zao za uganga ikiwemo kutoa ramli chonganishi ambao zinapelekea watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kuawa au kukatwa viungo.
Alitaja baadhi ya vitu vilivyokamatwa kuwa ni mikia mitano  ya Nyumbu,mavi ya Tembo, ngozi ya kenge,shanga sita, Pombe za Ng’ombe 6, gamba la Kombe, magamba ya Karunguyeye, chupa saba zenye dawa ya kienyeji, mifupa ya Nguruwe na gamba la Konokono,ngozi ya Simba na ya Nyegere.
“Kutokana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) yanayoendelea kujitokeza nchini hivi sasa, jeshi la polisi mkoani hapa limejipanga vizuri katika kukabiliana na waganga wanaopiga ramli chonganishi ambazo ndizo zinazochochea ukosefu wa amani na mauaji ya walemavu hao”,alisema Haule kwa kujiamini.
Katika hatua nyingine, alisema jeshi la polisi mkoa wa Singida linafanya sensa ya watu wenye ulemavu wa ngozi katika mkoa mzima,ili kuweza kujua idadi yao na kuweka ulizni juu yao ikiwa ni pamoja na mikakati ya kutoa seimna mbalimbali kwa waganga hao waweze kufanya kazi yao kuendana na wakati huu wa sayansi na teknolojia.
“Lengo ni kwamba wafanye kazi zao bila kujihusisha na ramli chonganishi na kwa njia hiyo tutakuwa tumetokomeza mauaji kwa ndugu zetu walemavu wa ngozi (albino)”,alifafanua.
Kuhusu watuhumiwa hao waliokamatwa,alisema kwa sasa wanaendelea na uchunguzi zaidi na baada ya kukamilika,watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayowakabili ya kufanya shughuli za uganga wa kienyeji bila kuwa na vibali.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo