Wafungwa 14 waliohukumiwa adhabu ya kifo
katika gereza la Isanga, mkoani Dodoma, wamelalamikia ucheleweshwaji wa
nakala za hukumu za kesi zao kwa zaidi ya miaka mitano, hali
inayowakwamisha kukata rufaa.
Kwa mujibu wa taarifa ya wafungwa hao
ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mashariki imekuwa na
ukiritimba katika utoaji wa nakala za hukumu za kesi na hivyo kushindwa
kukata rufaa wakati ni haki yao ya msingi.
Wafungwa hao (majina tunayahifadhi),
walisema Kanda ya Mashariki imekuwa na tatizo katika kushughulikia
suala hilo ukilinganisha na Mahakama Kuu za kanda nyingine ambazo
wafungwa wamekuwa wakipewa nakala za hukumu za kesi kwa ndani ya kipindi
cha mwaka mmoja.
“Sisi wafungwa wa adhabu ya kifo wa
gereza la Isanga Dodoma tunailalamikia kanda ya Mashariki hususan
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mashariki kwa kutucheweleshea milolongo
na nakala za hukumu za kesi zetu kwa zaidi ya miaka mitano tofauti na
kanda zingine zote ambazo hutoa nakala hizo ndani ya mwaka mmoja tu,”
wameeleza katika taarifa yao.
Waliongeza kuwaa ucheleweshaji huo wa
nakala za hukumu hupelekea kuchelewa kusikiliza rufani zao kwa zaidi ya
miaka kumi tofauti na kanda zingine rufaa husikilizwa ndani ya miaka
miwili tu.
“Baya zaidi maswahibu haya hutukumba
sisi tusio na pesa, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni, haki
inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa, tunamuomba Mwanasheria Mkuu, Jaji
Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria watutatulie kero hiyo kwani siyo wote
tulio gerezani tuna makosa,” wameeleza.
Wafungwa wanaolalamikia suala hilo ni
wale ambao walihukumiwa adhabu ya kifo kati mwaka 1992 ambao idadi yao
ni mmoja, 2003 (mmoja), 2004 (mmoja), 2007 (mmoja), 2009 (wawili), 2010
(watatu), 2011 (watatu) na mwaka 2012 wapo wawili.
