Kesi inayomkabili kiongozi wa jumuiya na taasisi za kiislamu nchini
Sheikh Ponda Issa Ponda imeendelea katika mahakama ya hakimu mkazi
mkoani Morogoro na upande wa utetezi umewasilisha hoja zitakazoifanya
mahakama kutoona sababu kwa mshtakiwa kuwa na kesi ya kujibu.
Mawasilisho hayo yamefanywa mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa
mahakama ya mkoa wa Morogoro Bi, Mary Moyo kwa zaidi ya saa tatu na
wakili Juma Nasoro pamoja na Abubakari Salimu wanaomtetea sheikh Ponda
ambapo katika mawasili hayo wakili Nasoro amedai ushahidi uliotolewa na
upande wa mashtaka pamoja na vielelezo vilivyotolewa mahakamani hapo
unatia shaka na unaudhaifu mkubwa unaomfanya mshitakiwa akose kesi ya
kujibu.
Aidha wakili Nasoro amedai kuwa hati ya mashtaka yenye makosa
matatu inaonekana kuwa na mapungufu hasa katika shtaka la kwanza kwani
imeshindwa kueleza ni kwa namna gani mshtakiwa huyo alikiuka amri halali
ya mahakama kama alivyoshitakiwa katika hati hiyo pamoja na hayo amedai
kuwa hukumu iliyotolewa mahakama ya kisutu dhidi ya mshitakiwa Ponda
haina amri yoyote inayoonesha kuwa imetengeneza kosa kwa sheikh Ponda
bali inaweza kuwa ni kukiuka masharti ambayo sio kosa la jinai.
Baada ya mawasilisho hayo upande wa mashtaka ukiongozwa na waliki
mkuu wa serikali Benard Kongola umeiomba mahakama kujibu hoja
zilizowasilishwa na upande wa utetezi ambazo zitathibitisha bila ya
kuwepo kwa shaka yoyote kama sheikh Ponda alivyoshtakiwa mahakamani hapo
ambapo mahakama imeridhia ombi hilo na kesi imeahirishwa hadi machi 20
na hivyo mshtakiwa kurudishwa rumande.