Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amesema ofisi yake ilijaribu kuazima vifaa vya kielektroniki vya Biometric Voters Registration (BVR) katika nchi ya Kenya na Nigeria kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura, lakini nchi hizo zilikataa.
Uamuzi wa NEC wa kutaka kuazima vifaa hivyo ni kutokana na mchakato wa uandikishaji kukwama kwenda kama ulivyopangwa kutokana na BVR 250 zilizopo kutokuwa na uwezo wa kuandikisha wapiga kura wote nchini.
Kitendo hicho kinaweza kusababisha Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30 mwaka huu kushindikana kwani mpaka sasa ni mkoa wa Njombe pekee uandikishaji unaendelea kufanyika ambako utamalizika Aprili 12, 2015.
“Tulitaka kuazima Kenya lakini wakasema wanavitumia hata kama wamemaliza uchaguzi lakini mchakato wao wa uandikishaji unaendelea kutokana na kwamba watu wao wanapofikisha umri wa kuandikishwa wanawaingiza katika daftari lao,” alisema JajiLubuva na kuongeza:
“Tulikwenda Nigeria nako walitueleza wanazitumia. Kuazimana siyo jambo geni kwetu na huu ndiyo ukweli wake.”
Kuhusu mchakato wa uandikishaji mkoani Njombe alikoweka kambi alisema: “Uandikishaji huku unakwenda vizuri licha ya kauli mbalimbali na mimi nimekuwa nikiwahamasisha kujitokeza na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.”
Katika uchaguzi wa Ghana uliofanyika mwaka 2013 mfumo wa BVR ulitumika na kuonyesha mafanikio makubwa. Hata hivyo, Malawi iliukataa mfumo huo katika uchaguzi wa mwaka 2014 baada ya kuonyesha udhaifu mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2005
