WAZEE wasiojiweza na watoto yatima walioko katika Kituo cha Kiilima
kilichoko Bukoba Vijijini, wamesema walilazimika kususa kula kwa siku
mbili mwezi uliopita baada ya kupata habari za kuondolewa kwa Mkuu wa
Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe.
Walitoa kauli hizo juzi wakati wakipokea zawadi za mwaka mpya,
walizokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella aliyechukua
nafasi ya Massawe kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete.
Evelyn Mshana ambaye ni mmoja wa wahudumu kituoni hapo, alisema mwezi
uliopita wahudumu wa kituo hicho walijikuta katika wakati mgumu baada
ya wazee kumi na watoto yatima 12 wanaolelewa hapo, kususa kula na
kububujikwa na machozi wakimlilia Massawe ambaye anasubiri kupangiwa
majukumu mengine na Rais Jakaya Kikwete.
“Siku ya kwanza, baada ya kupita saa tano tangu watangaze kutokula
wala kunywa chochote, uongozi wa kituo uliamua kukaa nao na baada ya
kuwahoji, walisema wamesikia kupitia vyombo vya habari kuwa mtu wao
ameondoka, hivyo wako kwenye huzuni.
“Jambo hilo sisi tuliliona la kawaida sana, lakini madhara yake
yalikuwa makubwa, unawaona wazee hawa wengine wana miaka zaidi ya 90
waliendelea na msimamo wa kutokubali kula chakula wala kunywa chochote
kwa siku mbili, tuliendelea kupata wakati mgumu mpaka tulipowabembeleza
sana na kuwaahidi kuwasiliana na mkuu wa mkoa huyo wa zamani ili
amshauri mkuu wa mkoa mpya aendelee kuwatembelea na kuwatafutia misaada
sambamba na kuibua miradi itakayowasaidia kama alivyokuwa akifanya
Massawe,” alisema Evelyn.
Mmoja wa wazee aliyeishi kituoni hapo kwa zaidi ya miaka 25,
Everister Kayogera, alipoulizwa sababu za kugoma kula na kuangua vilio
kituoni hapo, alisema Massawe alikuwa ni nguzo kubwa kwao kwani
aliwashauri mambo mengi ambayo yamewanufaisha kwa kipindi kifupi.
“Tunamshukuru Rais kwa kutukumbuka kila mwaka na kututumia zawadi za
mwaka mpya, kwanza tuliposikia kuwa mkuu wetu wa mkoa Massawe
amehamishwa tuliumia sana mpaka machozi yakatutoka huku tukiamua kulala
njaa na kushinda njaa mpaka aje tuongee naye, aweze kutuhakikishia kama
yale tuliyopanga naye yataendelea kutekelezeka,” alisema Kayogera.
Mzee mwingine ambaye pia ni mlemavu wa viungo, anayelelewa kituoni
hapo, Wilson Zikumana alisema kwa takribani miaka mitatu sasa, Massawe
aliwabadilishia mfumo wa maisha, kiasi cha kuwafanya wajishughulishe na
kufanya shughuli za uzalishaji, ikiwa pamoja na kilimo ambacho
kinawawezesha kujitegemea kwa kiasi kikubwa kwa chakula.
Alisema walikuwa pia na mipango mingi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha
ufugaji. Kutokana na hali hiyo, walimshauri Mongella kuhakikisha anafika
kituoni hapo mara kwa mara na kusaidia kutatua changamoto
zinazowakabili hasa ya ukosefu wa huduma ya afya.