MKURUGENZI Mdhibiti Uchumi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Dk
James Diu, amejichanganya mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa
Umma, kuhusu matumizi halisi ya fedha alizozipokea kutoka kwa James
Rugemalira ambazo ni Sh milioni 80.8.
Akijitetea mbele ya baraza hilo, Mkurugenzi huyo ambaye pia aliwahi
kushika wadhifa wa Meneja Udhibiti Uchumi katika Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (EWURA), alikiri kupokea kiasi hicho cha fedha ambacho
alidai alikitumia kwa ajili ya matibabu ya mkewe aliyefariki dunia
Agosti mwaka jana kwa ugonjwa wa saratani.
Hata hivyo, katika maelezo yake aliyoyatoa mbele ya Kamati ya
Uchunguzi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na tamko lake
la mali na madeni alilolitoa Desemba 30, mwaka jana katika Sekretarieti
hiyo, kiongozi huyo alibainisha kutumia kiasi hicho cha fedha katika
kulipia deni lake la nyumba alilokuwa akidaiwa.
Awali Wakili wa Sekretarieti hiyo ya maadili, Wemaeli Mtei, akimsomea
mashtaka mkurugenzi huyo, alidai kuwa mlalamikiwa huyo anadaiwa kuomba
na kupokea Sh milioni 80.8 kutoka kampuni ya VIP Engineering and
Marketing Limited kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alisema pamoja na fedha hizo, pia mlalamikiwa huyo anadaiwa kujipatia
maslahi ya kiuchumi kwa kupokea kiasi cha dola za Marekani 25,000
kutoka kampuni ya Mabibo Beers, Wine and Spirit mali ya Rugemalira,
kinyume cha Sheria hiyo ya maadili, inayokataza kiongozi wa umma kuomba
na kupokea maslahi binafsi.
Aidha katika hati hiyo ya mashtaka mlalamikiwa huyo pia anadaiwa
kupokea dola za Marekani 10,100 kutoka Kampuni ya Prime Fuel Tanzania
Limited ambazo zote hakuzitamka kama Sheria hiyo ya maadili inavyotaka.
“Mlalamikiwa ambaye pia kuanzia mwaka 2006 hadi 2011 aliwahi
kufanyakazi katika taasisi ya Serikali ya Ewura inayoshughulika na
masuala ya nishati, alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kampuni ya
VIP yenye hisa asilimia 30 na kampuni ya IPTL yenye mkataba wa umeme na
Tanesco, jambo linalosababisha mgongano wa kimaslahi,” alisema Mtei.
Shahidi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Zahara Guga,
alisema kitendo cha mlalakiwa kuwa na historia ya kufanya kazi EWURA na
kupokea fedha kutoka kampuni ya VIP ambayo inasimamiwa na mamlaka hiyo
ni kinyume na Sheria ya maadili na pia mgongano wa kimaslahi.
Alisema katika uchunguzi wa kamati hiyo ya uchunguzi, walibaini kuwa
mlalamikiwa alifungua akaunti Februari 4, mwaka jana na kuingiziwa Sh
milioni 80.8 Februari 5, mwaka huo na kampuni ya VIP katika akaunti yake
iliyopo benki ya Mkombozi tawi la Kariakoo.
Akijitetea mbele ya baraza hilo, Dk Diu, alikanusha kuomba fedha hizo
kwa Rugemalira na kukiri kuwa alipokea kiasi hicho cha fedha ambazo
alipatiwa kama ahadi ya kumsaidia katika matibabu ya mkewe, ikiwa ni
pamoja na kumsafirisha kwenda India kwa matibabu zaidi.
“Rugemalira ni rafiki yangu wa karibu pamoja na familia yangu, lakini
pia nimesoma naye wakati natafuta shahada yangu ya kwanza Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, mwaka 1982 hadi 1985, alinipatia fedha hizi kama
ahadi sijamuomba, kudai wala kupokea maslahi ya kiuchumi kutoka kwake,”
alisisitiza.
Alisema kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo mkewe, Rugemalira
alikwenda kumjulia hali alipolazwa hospitali ya TMJ na baadaye
Sanitarius iliyopo Mikocheni ndipo alipoahidi kutoa fedha hiyo kama
mchango na msaada wa matibabu na baadaye mazishi baada ya mkewe huyo
kufariki dunia.
Aidha alisema hata katika fomu yake ya tamko la mali na madeni kwa
sekretarieti hiyo, aliyoiwasilisha Februari 30, mwaka jana aliitamka
fedha hizo kuwa ameipokea kutoka kwa Rugemalira.
“Awali sikuona umuhimu wa kuiwasilisha kwa ofisa masuhuli wangu kwa sababu haikuwa zawadi na sikuona umuhimu wa kufanya hivyo,”.
Aidha alisisitiza kuwa kupokea kwake fedha hizo hakuna mgongano
wowote wa kimaslahi kwa kuwa hana uhusiano wowote wa kibiashara na
Rugemalira na hata kazi yake katika mamlaka ya TCAA haina uhusiano na
kampuni za Rugemalira kibishara.
Hata hivyo, baadaye akionesha maelezo ya Dk Diu mbele ya kamati ya
uchunguzi alipohojiwa kuhusu kupokea fedha hizo, Wakili wa Sekretarieti
hiyo ya Maadili Getrude Cyriacus, alibainisha kuwa mlalamikiwa huyo
alijitetea kuwa fedha hizo alizitumia kulipia deni la nyumba alilokuwa
akidaiwa.
“Hata katika tamko la mali na madeni aliloliwasilisha mwaka 2012,
aliandika maelezo kuwa anadaiwa Sh milioni 80 za nyumba ambayo
haijakamilika aliyonunua huko Mbezi kutoka kwa Godson Shangwe, na tamko
lake la mwaka jana alibainiha kuwa ametumia fedha hizo alizopewa na
Rugemalira kumalizia deni hilo,” alisema Cyriacus.