Inasikitisha: Bibi Asimulia Mvua Ilivyoua Wajukuu Zake Wanne na Wengine 38 Kahama

Maafa makubwa yameikumba Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga baada ya watu 42 kufa papo hapo na wengine 82 kujeruhiwa, kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali,  iliyonyesha katika Kijiji cha Mwakata Kata ya Isaka.

Kamanda wa  Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema jana kuwa tukio hilo halijawahi kutokea mkoani humo.
 
Baadhi ya majeruhi, akiwemo Paulina Malongo aliyefiwa na wajukuu wanne, walieleza hali ilivyokuwa.
 
Shughuli za uokoaji ziliendelea hadi jana chini ya Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, ambapo  Mkuu wa Wilaya ya Kahama,  Benson Mpesya alisema huenda idadi ya waliokufa na majeruhi, ikaongezeka.
 
Kamanda alisema mvua hiyo iliyosababisha maafa, ilinyesha juzi saa 3 usiku katika kijiji hicho ikiambatana na upepo mkali ulioangusha miti, kubomoa na kuezua nyumba, hivyo kusababisha vifo na majeruhi hao.  Inadaiwa wengi waliopoteza maisha ni watoto.
 
Baadhi ya majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama, walisema mvua ilikuwa kubwa ikiambatana na upepo mkali. Walisema nyumba zilizoezuliwa na wakati huo huo upepo uling’oa miti.
 
“Tulikuwa tumelala majira ya saa tatu usiku ghafla tulisikia upepo mkali ukiambatana na mvua kubwa ya mawe. Maji mengi yaliingia ndani na ghafla nyumba yangu ilianguka na nimepoteza wajukuu wangu wanne,” alisema Paulina Malongo, ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho cha Mwakata.
 
Kamanda Kamugisha alisema majeruhi walikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa ajili ya kupatiwa matibabu wakati jitihada zaidi za uokozi zikiendelea katika kijiji hicho.
 
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama,  Dk Joseph Ngowi akizungumza na waandishi wa habari, alisema amepokea majeruhi zaidi ya 60 na kati yao  watatu walifariki wakati wakiendelea na matibabu hospitalini hapo.
 
“Hatuna idadi kamili ya watu waliojeruhiwa au waliokufa na tumetuma madaktari wetu kwenda katika kijiji hicho kwa ajili ya huduma ya kwanza pamoja na kufanya uchunguzi ili kubaini idadi kamili ya waliofariki dunia,” alisema Ngowi.
 
Dk  Ngowi alisema  kutokana na umbali uliopo kutoka eneo la tukio hadi hospitali ya wilaya, wamelazimika kutuma jopo la madaktari kwenda eneo la tukio, kubaini waliofariki na kuidhinisha maziko kupunguza gharama kwa wananchi waliofiwa.
 
Mkuu wa Wilaya ya Kahama,  Benson Mpesya alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ilitegemea kukaa jana mchana kutathimini takwimu za uharibifu wa mali na idadi ya nyumba zilizokumbwa na maafa .
 
Mpesya alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  kwa kushirikiana na wananchi,  wanaendelea na shughuli za uokoaji na huenda idadi ya waliokufa  pamoja na majeruhi ikaongezeka katika tukio hilo.
 
Watu wapatao 3,500 wameathiriwa na maafa hayo katika Kata  ya Mwakata. Kwa upande wa kaya zilizoathirika, 350 ni  za Kijiji cha Makata, 100 za Kijiji cha Ngumbi na kaya 50 za Kijiji cha Magung’hwa.
 
Athari zilizobainika papo hapo ni nyumba kadhaa, kuezuliwa na nyingine kubomoka, hali ambayo imesababisha kaya husika kukosa mahali pa kuishi. Aidha chakula cha akiba katika kaya hizo,  kimeharibika na kingine kusombwa na maji.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo