WIZARA ya Elimu na Ufundi imesema itazifutia usajili shule zote za serikali au binafsi, zitakazobainika kukaidi agizo la wizara hiyo lililotolewa wiki iliyopita la kuacha kuweka viwango maalumu na tofauti za ufaulu kutoka kidato kimoja kwenda kingine.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Anne Kilango alisema wizara hiyo inaendelea na uchunguzi na kufungia shule zote hata kama zinamilikiwa na wabunge wanatakiwa kufuata sheria.
Kilango alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) aliyetaka kujua hatua za serikali kwa shule zinazoendelea kukaidi agizo hilo, ikiwa ni pamoja na Sekondari ya Stanley ambayo inataka wanafunzi kupata wastani 50.
Huku akitaka serikali kuweka kiwango elekezi kwa ajili ya shule zote ili kuepuka kuweka kiwango kingine cha asilimia 60 . Akijibu swali hilo, Kilango alisema Wizara baada ya kutoa onyo wiki iliyopita haitatoa nyaraka tena, bali itafanya uchunguzi na kufutia usajili shule zote zitakazokaidi hata zikiwa za wabunge.
Akizungumzia kiwango elekezi alisema walimu wanapaswa kutambua kuwa wanafunzi wana uelewa tofauti, hivyo alama ya ufaulu ni asilimia 30 inayotumika kwa kidato cha pili hivyo wanatakiwa kuwasaidia wale wenye uelewa mdogo kwa walimu kuweka programu za kuwasaidia.
Katika swali la msingi, Selasini alitaka kufahamu iwapo serikali inaunga mkono uwekaji wa alama maalumu ya ufaulu kutoka kidato kimoja hadi kingine kwa shule zisizo za serikali.
Alihoji iwapo utaratibu huo unakubalika, kwa nini serikali isiweke kiwango maalumu na shule inapomkataa mwanafunzi sio kukwepa majukumu ya malezi, unyanyasaji wa kisaikolojia na kuzingatia biashara zaidi kuliko elimu.
Akijibu swali hilo, Kilango alisema serikali haiungi mkono utaratibu huo kwa kuwa umekiuka nyaraka za Elimu, Waraka wa Elimu namba 12 wa mwaka 2011 na Waraka wa Elimu namba 4 wa mwaka 2012 hivyo atakayekiuka agizo la Waziri wa Elimu Shukuru Kawambwa alilotoa wiki iliyopita kuhusu suala hilo atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Alisema Waraka wa Elimu Namba 6 wa mwaka 2011, umetoa maelekezo kuhusu wastani wa ufaulu katika mtihani wa kidato cha pili ambapo kiwango cha alama ya ufaulu ni asilimai 30 tu na si vinginevyo kwa shule za serikali na binafsi.
“Napenda kulihakikishia Bunge kwamba utaratibu huu uliowekwa na shule za serikali haukubaliki na serikali,” alisema.