Mtuhumiwa Aliyeua Polisi kwa Panga naye Auawa na Wananchi.....Polisi Yawapongeza wananchi kwa Uamuzi huo

Mtuhumiwa Tissi Mallya ambaye alitoroka baada ya kumuua askari Polisi G.7168 Koplo Joseph Swai, ameuawa usiku wa kuamkia jana na wananchi alipokuwa amejificha akiwa na panga lenye damu, lililotumika kwenye mauaji hayo.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, alisema mauaji hayo yalitokea juzi asubuhi katika eneo la Chang’ombe Juu.
 
Kamanda Misime alisema baada ya Malya kutekeleza mauaji hayo alikimbia, lakini ilipofika majira ya saa 5 usiku wananchi walimuona maeneo ya Mtimkavu Mailimbili akiwa bado na panga alilotumia kumuua Koplo Joseph.
 
“Wananchi walichukua sheria mkononi na kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake, polisi walifika eneo la tukio na kumchukua kisha kumkimbiza Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma lakini aligundulika tayari amefariki”, alisema.
 
Kamanda Misime alisema katika kumbukumbu walizonazo ni kuwa mwaka 2006 Malya aliwahi kufungwa miaka mitatu kwa kosa la kujeruhi, pia mwaka 2009 alifungwa tena miezi sita kwa kosa la kutishia kuua.
 
“Nawapongeza wananchi walioonesha kuchukizwa na kitendo alichotendewa askari wetu lakini waache kujichukulia sheria mkononi,”alisema.
 
Pia, alitoa wito kwa wananchi kuanza kuchukua hatua kurekebisha maadili kuanzia ngazi ya familia, kwani imebainika mtuhumiwa alikuwa mvuta bangi, kiasi cha kumfanya awe anafanya vitendo ambavyo ni kinyume na maadili wa nchi.
 
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Mnadani Steven Masangia alisema alifahamu Koplo Joseph Swai kama kijana mchapakazi, ambaye alijitolea kutoa elimu hata kwenye mitaa juu ya ulinzi shirikishi.
 
Alisema Jeshi limempoteza kijana shupavu, ambaye alikuwa nguzo na kiungo kikubwa katika watu wa rika zote.
 
“Alipokuwa Mnadani, alipambana kuhakikisha uhalifu unakomeshwa na hata vijana wanaovuta bangi aliwasambaratisha, na alikuwa akifundisha polisi jamii kwenye mitaa ya kata”, alisema.
 
Alisema kijana huyo alikuwa mchapakazi na alikuwa akiipenda kazi yake na amekufa kama shujaa. “Alikuwa na cheo kidogo, lakini kazi alizokuwa akifanya zilikuwa ni kubwa kulinganisha na cheo na umri wake,” alisema .
 
Katika mkasa huo, uliotokea juzi asubuhi, askari huyo aliitikia wito uliofika kwake wa kuwapo kwa dalili ya tendo la jinai nyumbani kwa mkazi mmoja wa Chang’ombe Juu .
 
Katika taarifa yake ya awali, Kamanda Misime alisema askari huyo alipigiwa simu na Mtendaji wa Mtaa wa Chang’ombe Juu akimjulisha kuwa amepokea taarifa ofisini kwake kutoka kwa Oliver Baltazar (52) mkazi wa Chang’ombe Juu kuwa mtoto wake aitwaye Tisi Sirili anaonekana anataka kumuua au ameshamuua mtoto wake wake wa miezi minane, Valerian Tisi.
 
Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo askari huyo alienda ofisini kwa Mtendaji huyo ambapo waliongozana hadi nyumbani kwa mtuhumiwa.
 
“Alipofika askari aligonga mlango huku akijitambulisha kuwa yeye ni askari ili mtuhumiwa atoke nje, alichofanya mtuhumiwa ni kumnyanyua mtoto wake mdogo wa miezi minane kwa mkono mmoja kichwa chini miguu juu na kutaka kumkata kwa panga huku akisema, namkata shingo na sitaki kuona mtu. 
  
“Askari aliamua kumuokoa mtoto huyo kwa kumrukia mtuhumiwa lakini kwa bahati mbaya aliteleza na ndipo mtuhumiwa akamkata kichwani askari wetu,”alisema Misime.
 
Aidha alisema, pamoja na askari huyo kuanguka mtuhumiwa aliendelea kumkatakata kwa panga huku Mtendaji na kijana aliyekwenda naye katika eneo la tukio, wakikimbia huku wakipiga kelele za kuomba msaada.
 
Alisema mtuhumiwa baada ya kufanya kitendo hicho cha kinyama, alikimbia akiwa na panga lake huku nguo zake zikiwa zimetapakaa damu.
 
Wakati huohuo, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu jana aliongoza mamia ya wakazi wa Dodoma kumuaga askari Polisi huyo, Koplo Joseph Swai (27) ambaye tayari amesafirishwa kwenda Arusha kwa maziko.
 
Alisema Jeshi la Polisi linatakiwa kuongeza kasi ya kupambana na uhalifu, kutokana na kuongezeka kwa vitendo hivyo ndani ya jamii.
 
“Kijana amekufa kishujaa wakati akitetea mtu asiye na uwezo wakati akinyanyaswa, katika kifo hiki askari wapate cha kujifunza kwani kimewatia nguvu na kuwawezesha kufahamu namna ya kukabiliana na uhalifu. Msiba huo ni fursa ya kujihami na kukomesha uhalifu,” alisema.
 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa alisema ni wajibu wa jamii kufichua wahalifu ili waweze kukabiliana na mikono ya sheria.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo