Wajawazito wakazi wa kata za Sululu na Matawale katika Halmashauri ya Mji wa Masasi mkoani Mtwara, wamekuwa wanajifungua kwa kutumia vibatari muda wa usiku zaidi ya miaka mitano sasa.
Diwani wa Kata ya Sululu, Peter Mrope alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Alisema
kuwa hali ya zahanati sio nzuri na zaidi ya miaka mitano wakazi wake na
kata ya jirani ya Matawale, wanapougua au kujifungua wakati wa usiku,
wauguzi na madaktari wanatumia vibatari ili wapate kumhudumia mgonjwa
aliyefika muda huo.
Alisema zahanati hiyo iliyopo kijiji cha Makalani, haina huduma za umeme au nishati ya jua, kiasi huduma za afya kuzorota.
Mrope alisema baadhi ya wauguzi na watumishi hawaipendi zahanati hiyo, kutokana miundombinu yake sio rafiki kwa watumishi.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, Andrew Mtumisha alikiri kuwapo tatizo
la ukosefu wa huduma ya umeme, linalosababisha wajawazito na wagonjwa wa
magonjwa mbalimbali kutibiwa kwa kutumia vibatari katika zahanati ya
Sululu.
Alisema
tatizo hilo ni la muda mrefu. Alisema hakuna miundombinu ya umeme
tangu zahanati ikiwa katika Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani
Mtwara.
Alisema
baada ya kugawa maeneo ya mipaka na utawala kati ya Halmashauri ya
Mji na Halmashauri ya wilaya, kata ya Sululu ilipangwa kuwa ya
Halmashauri ya Mji wa Masasi mwaka 2012.
Alisema
kipindi hicho, Mfuko wa Jimbo ambao uko chini ya Mbunge wa jimbo
ulishaanza, lakini zahanati hiyo haijapata nishati ya jua ili kuondoa
tatizo la wagonjwa kujifungua kwa kutumia vibatari.
Alisema
ofisi ya Mbunge na Uongozi wa Mfuko wa Jimbo, unapaswa kukagua
maendeleo ya zahanati hiyo na kuweza kubaini tatizo hilo.
Alisema
kikao cha Baraza la Madiwani cha Januari 30, mwaka huu kiliagiza Ofisi
ya Mkurugenzi kununua na kuweka umeme wa jua kwa muda wa mwezi mmoja.
Mkurugenzi
wa Mji wa Masasi, Fortunatus Kaguro alikiri kupewa maazimio ya kwenye
kikao cha Baraza la Madiwani kununua nishati ya jua.